UEFA-ATLETICO MADRIDI-REAL MADRID-SOKA

Atletico Madrid wailaza Real Madrid 4-2

Mashabiki wa Atletico Madrid wakisherehekea ushindi wa klabu yao.
Mashabiki wa Atletico Madrid wakisherehekea ushindi wa klabu yao. REUTERS/Juan Medina

Klabu ya Atletico Madrid wamewaadhibu wapinzani wao wa jadi Real Madrid mabao 4-2 katika michuano ya Kombe la Super Cup ya UEFA. Real Madrid wamecheza mechi hiyo miezi kadhaa baada ya meneja wao Zinedine Zidane kuachia ngazi.

Matangazo ya kibiashara

Hadi dakika tisini za mchezo timu zote mbili zilikua sare ya kufungana 2-2. Atletico Madrid imeshinda mechi hiyo baada ya kupata mabao mawili katika muda wa ziadamabao ambao yalifungwa na wachezaji Koke na Saul.

Nyota wa zamani wa Chelsea Diego Costa alikuwa amewafungia Atletico mabao mawili muda wa kawaida.

Bao la kwanza liliingizwa sekunde 49 baada ya mechi kuanza na la pili kipindi cha pili. Diego Costa alijizolea sifa nyingi na umaarufu katika mechi hiyo dhidi ya Real Madrid.

Ilikuwa mechi ya kwanza ya ushindani kwa Real Madrid tangu mchezaji nyota wa zamani Ronaldo alipohamia Juventus ya Italia majira ya joto, ambapo alinunuliwa kwa euro milioni 99.

Real Madrid walishindwa mechi hiyo baada ya kuondoka kwa Zidane ambaye nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa meneja wa timu ya taifa ya Uhispania Julen Lopetegui.

Atletico walishinda Super Cup kwa mara yao ya tatu na kuhakikisha kwamba hawajawahi kushindwa katika mechi za Super Cup kwani wameshiriki mara tatu.

Karim Benzema aliifungia timu yake ya Real Madridi bao la kwanza kupitia mchezaji Gareth Bale kabla ya nahodha wao Sergio Ramos kufunga penalti na kuwaweka kifua mbele 2-1 kwa muda baada ya Juanfran kuadhibiwa kwa kunawa mpira eneo la hatari.

Beki kamili Marcelo alipoteza nafasi ya kuwafungia Real bao la ushindi sekunde za mwisho za muda wa kawaida mechi hiyo, na kuwapotezea mabingwa hao wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya nafasi ya kuwa klabu ya kwanza ya kushinda kombe hilo mara tatu mfululizo.