SOKA-TANZANIA-SIMBASC-YANGASC

Kwanini TFF imetangaza mapema viingilio vya mchezo wa Simba na Yanga?

Mashabiki wa klabu za Simba na Yanga
Mashabiki wa klabu za Simba na Yanga RFI Kiswahili

Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF umetangaza viingilio vya mchezo wa watani  wa jadi Simba na Yanga utakaochezwa Septemba 30 katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Simba na Yanga zitachuana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu wa mwaka 2018/19.

Ofisa wa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Ndimbo ameeleza wanahabari kwamba mchezo uko palepale na wamelkazimika kutoa taarifa mapema ili kuhakikisha mchezo huo unachezwa kwa usalama mkubwa.

"Tiketi zitaanza kuuzwa kuanzia Septemba 20, na tiketi zitapatikana kupitia kadi za Selcom,"ameeleza Ndimbo.

Kiingilio cha chini kitakuwa shilingi 7000, V.I.P B na C shilingi 20,000 na V.I.P A kiingilio chake ni shilingi 30,000.

Hata hivyo, swali linabaki kwanini TFF inautazama kwa jicho pana mchezo huu?

Simba na Yanga ni klabu zenye mashabiki wengi na ambao hupenda kushuhudia mchezo huu kuliko mchezo mwingine wowote katika Ligi ya Tanzania.

Mwandishi wa michezo wa RFI Kiswahili anakubaliana na uamuzi wa TFF kutangaza mapema viingilio vya mchezo huo ili mashabiki wengi wenye shauku ya kutazama mchezo huo wafanye hivyo.

Pili uwepo wa wachezaji wapya waliosajiliwa na klabu hizo kama Meddie Kagere, Pascal Wawa ambao wameanza vizuri kwa upande wa Simba, Deus Kaseke na Makambo kwa upande wa Yanga pia wanaongeza mvuto kwa mchezo huo.

Aidha, kiusalama, hatua ya TFF kutangaza mapema uratibu wa mchezo huo unatoa nafasi kwa vyombo vya usalama hususani Jeshi la Polisi kujipanga kuhakikisha usalama unaimarishwa kabla, wakati na baada ya mchezo huo ili kuepusha matukio ambao yanaweza kuhatarisha amani.

Oktoba mosi, 2016 katika mchezo baina ya timu hizo kulishuhudia matukio ya uvunjifu wa amani, mojawapo ya geti la kuingilia uwanjani hapo liling'olewa na mashabiki na pia mashabiki wa Simba walivunja viti kwa madai ya kutoridhishwa na uchezeshaji wa mwamuzi Martin Sanya.

Kwa ujumla mazingira yanayouzunguka mchezo wa Simba na Yanga, ndiyo yanatoa funzo kwa mamlaka zinazohusika kuchukua tahadhari mapema.