SIMBASC-YANGASC=SOKA=TANZANIA

Mashabiki wa soka Tanzania wasubiri kwa hamu mchezo wa Simba na Yanga

Mashabiki wa Simba na Yanga wakitambiana nje ya Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam
Mashabiki wa Simba na Yanga wakitambiana nje ya Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam

Mashabiki wa Soka nchini Tanzania kesho watashuhudia mchezo wa wapinzani wa jadi Simba na Yanga.

Matangazo ya kibiashara

Mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara itachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania Jonesia Rukya.

Mechi ya Simba na Yanga ni mojawapo ya dabi kubwa Afrika, ikitajwa kulinganishwa na mchezo baina ya Zamalek na Ahly nchini Misri, Kaizer Chiefs na Orlando Pirates nchini Afrika Kusini au Gor Mahia na AFC Leopards nchini Kenya.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa imeshapoteza mechi moja dhidi ya Mbao wakati wapinzani wao Yanga wataingia dimbani wakijivunia ushindi katika mechi zao nne za kwanza za Ligi Kuu.

Makocha Mwinyi Zahera kwa upande wa Yanga, Patrick Aussems kwa upande wa Simba watakuwa wakiziongoza timu zao kwa mara ya kwanza katika mechi ya watani wa jadi.

Mwiba kwa Simba ni washambuliaji Haritie Makambo na Amiss Tambwe aliyefunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Singida United wakati washambuliaji Meddie Kagere na Emanuel Okwi wanatazamiwa kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Yanga.

Je ni Yanga yenye alama 12 itaifunga Simba na kupaa kileleni au ni Simba itakayoibuka na ushindi?

Majibu ya maswali haya, yatapatikana baada ya kumalizika dakika tisini za mchezo huo.