MBAO-GOR MAHIA-SOKA

Mbao FC yailaza Gor Mahia kupitia mikwaju ya penalti

Klabu ya Kenya ya Gor Mahia.
Klabu ya Kenya ya Gor Mahia. Twitter. com/ Gor Mahia

Mabingwa watetezi wa taji la SportPesa, Gor Mahia ya Kenya, wameondolewa katika michuano hiyo, baada ya kufungwa na Mbao FC ya Tanzania kwa mabao 4-3 katika mechi ya mwondoano, kupitia mikwaju ya penalti.

Matangazo ya kibiashara

Mchuano huo uliopigwa Jumatano mchana katika uwanja, wa Taifa jijini Dar es salaam, ulifika katika hatua hiyo baada ya kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Matumaini ya Gor Mahia kusonga mbele yalivunjika baada ya penalti ya nahodha Harun Shakava kuokolewa na kipa wa Mbao FC Metacha Mnata.

Wachezaji wa Gor Mahia waliofunga mabao ni pamoja na Francis Kahata, Jacques Tuyisenge na Boniface Omondi huku Said Hamis, Ngalema, Ibrahim Hashimu na David Mwasa wakiifungia Mbao FC.

Mbali na Gor Mahia, wawakilishi wengine wa Kenya AFC Leoaprds, nao wameondolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa na mabingwa wa soka nchini Tanzania Simba FC bao mabao 2-1.

Kuelekea katika michuano ya nusu fainali, klabu za Tanzania zilizofuzu ni pamoja ni Mbao, Simba huku Kenya ikiwakilishwa na timu za Bandari na Kariobangi Sharks.