UEFA-ULAYA-BARCELONA-BAYERN MUNICH-SOKA-MASHABIKI

UEFA: Mechi za mwisho kutafuta nafasi ya kucheza robo fainali

Mshambuliaji wa klabu ya Barcelona Lionel Messi
Mshambuliaji wa klabu ya Barcelona Lionel Messi Reuters/John Sibley Livepic

Klabu ya Bayern Munich kutoka Ujerumani, itakuwa mwenyeji wa Liverpool ya Uingereza katika mechi ya mzunguko wa pili, kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya, UEFA.

Matangazo ya kibiashara

Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Allianz Arena, kuanzia saa tano usiku saa za Afrika Mashariki.

Klabu zote mbili zinakwenda katika mechi hii, baada ya mechi ya kwanza, klabu  kutofungana. Mechi hiyo ilimalizika 0-0.

Mabingwa wa zamani Barcelona ya Uhispania, watakuwa nyumbani katika uwanja wao wa Camp Nou kumenyana na Lyon ya Ufaransa. Mechi ya kwanza, klabu zote mbili hazikufungana, zilitoka 0-0.

Siku ya Jumanne usiku, Manchester City ya Uingereza na Juventus ya Italia ilifuzu katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kupata ushindi mkubwa.

Wakicheza nyumbani katika uwanja wa Etihad, Manchester City waliifunga Schalke 04 ya Ujerumani kwa mabao 7-0 na kusonga mbele  kwa jumla ya mabao 10-2.

Juventus nayo, ilipata ushindi wa mabao 3-0 na kuilemea Atletico Madrid kwa jumla ya mabao 3-2. Mabao yote yalifungwa na  mshambuliaji Christiano Ronaldo, ambaye amesema alisajiliwa na klabu hiyo kufunga mabao.

Klabu ambazo zimefuzu katika hatua ya robo fainali ni pamoja na Manchester City, Manchester United, Tottenham Hotspurs zote za Uingereza, Juventus ya Italia, Ajax ya Uholanzi na Porto ya Ureno.