Vettel aionya timu ya Ferrari wakati Hamilton akishinda mbio za Monaco
Dereva wa kampuni Ferrari, Sebastian Vettel ameionya timu yake kuwa wanayo kazi kubwa ya kufanya mbele yao baada ya kushuhudia kwa mara nyingine wakimaliza katika nafasi ya pili kwenye mbio za Monaco.
Imechapishwa:
Akizungumza na wanahabari baada ya kumalizika kwa mbio hizo ambazo zilishuhudia ushindani mkali, bingwa huyo mara nne wa mashindano ya langalanga, ameeleza kuridhishwa na nafasi aliyomaliza.
Hata hivyo mbali na kueleza furaha aliyonayo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili, Vettel ameeleza kusikitishwa na namna dereva mwenzake Charles Leclerc alishindwa kumaliza mbio za hapo jana.
Mbio za Monaco zilishuhudia dereva wa kampuni wa Mercedes, Lewis Hamilton akimaliza katika nafasi ya kwanza licha ya kuwa alitumia matairi ambayo yalihatarisha nafasi yake.
Baada ya ushindi wake Hamilton alisema ushindi wake ni zawadi kwa mkongwe wa mbio hizo aliyefariki juma lililopita Niki Lauda ambaye alikuwa akifanya kazi na Mercedes na alikuwa na ushawishi mkubwa kwa Hamilton.
Katika kipindi cha karibu miaka miwili mfululizo, kampuni ya Ferrari imekuwa haifanyi vizuri huku wenzao wa Mercedes wakiendelea kuongeza alama na kuboresha magari yao.