CAF

Zamalek bingwa mpya kombe la shirikisho barani Afrika

Wachezaji wa timu ya Zamalek ya Misri wakishangilia ushindi hivi karibuni, 2019.
Wachezaji wa timu ya Zamalek ya Misri wakishangilia ushindi hivi karibuni, 2019. REUTERS/Amr Abdallah Dalsh

Penati za kiwango cha juu zilizopigwa na wachezaji wa klabu ya Zamalek ya Misri zilitosha kuipa ubingwa timu hiyo na kufanikiwa kumaliza ukame wa kutwaa taji kubwa barani Afrika uliodumu kwa karibu miaka 16, ambapo imefanikiwa kutwaa kombe la shirikisho barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Bao la dakika ya 55 la Mahmoud Alaa alilofunga baada ya kupitiwa kwa video maarufu kama VAR, lilitosha kuipa ushindi Zamalek na kufanya kulingana mabao na klabu ya Renaissance Sportive Berkane ya Morocco ambapo katika mchezo wa kwanza zilitoka sare ya bao 1-1.

Huku kukiwa hakuna sheria ya muda wa nyongeza katika michuano inayosimamiwa na CAF, timu hizo zililazimika kupigiana matuta ambapo Zamalek ilipata penati zote 5 huku Berkane ikipata mabao 3.

Penati waliyopata Zamalek kipindi cha pili na zile ambazo walipiga katika njia ya matuta, zilipigwa kwa ufundi wa hali ya juu na kumfanya mlinda mlango Abdelali Mhamdi kushindwa kunyakua penati hata moja.

Baada ya kushinda mataji ya CAF mwaka 1984 na 2003, klabu ya Zamalek ilishindwa kupta taji jingine hadi ilipofanikiwa kuishinda Berkane katika mechi ambayo hata hivyo ilichelewa kuanza.

Klabu ya Al Ahly ambayo ni jirani na Zamalek na ni wapinzani wa kubwa jijini Cairo kwa zaidi ya mwongo mmoja, imeshinda mataji 19 ya Afrika ikifuatiwa na klabu ya TP Mazembe ya Drc yenye mataji 11.

Kocha wa Zamalek ambaye aliwahi kukipiga na klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza Christian Gross raia wa Sweden, anakuwa kocha wa pili kutoka kwenye taifa hilo kushinda taji la shirikisho kama alivyowahi kufanya mwenzake Michel Decastel mwaka 2007 akiwa na klabu ya Tunisia.