UINGEREZSOKA-MICHEZO

Vilabu kuruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji 5 katika mechi

Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kuanza tena Juni 17 baada ya miezi mitatu ya kuwa imesitishwa.
Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kuanza tena Juni 17 baada ya miezi mitatu ya kuwa imesitishwa. EG Focus/Wikipédia

Timu zinazoshiriki ligi kuu ya Uingereza, sasa zitakuwa na uwezo wa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano, badala ya watatu kama ilivyozoeleka katika mechi, mabadiliko ambayo yataenda hadi mwishoni mwa msimu, baada ya vilabu kuidhinisha sheria hizi mpya.

Matangazo ya kibiashara

Katika sheria hizi mpya, timu pia itaruhusiwa kutaja orodha ya wachezaji tisa wa akiba badala ya saba kama ilivyokuwa awali.

Waandaaji wa sheria za michezo za kimataifa, walitoa ruhusa ya kuwepo kipengele cha kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba ili kulinda afya za wachezaji wakatik huu michezo ikianza kurejelewa tena barani Ulaya.

Ligi kuu ya Uingereza inatarajiwa kuanza tena Juni 17 baada ya miezi mitatu ya kuwa imesitishwa.

Licha ya kuwa timu sasa zitaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano, zitaruhusiwa kufanya mabadiliko mara tatu katika muda wa mchezo ili kuepusha mechi kusimama mara kwa mara kuruhusu mabadiliko.

Vilabu pia vimekubaliana kutumia uwanja huru ikiwa itahitajika, licha ya kuwa mechi karibu zote zinatarajiwa kuchezwa kwenye viwanja vyao ili kukabiliana na maambukizi ya Corona.

Katika makubaliano haya, pia idadi ya mashabiki katika kila mechi inaarifiwa kuwa haitazidi watu 300.

Mjadala mwingine uliokuwepo kati ya waandaaji wa sheria na vilabu ulikuwa ni kuhusu uwezekano wa bingwa kutangazwa mapema, kupata mshindi wa pili nakadhalika ikiwa ligi itasimama tena, uamuzi ambao hata hivyo umeahirishwa vilabu vikitaka kwanza ligi kurejea.

Bodi ya kimataifa ya mchezo wa mpira wa miguu, ilisema mwezi meo kuwa kutakuwa na mabadiliko ya muda kutokana na msimu wa mwaka 2019 na 2020 kuathiriwa kutokana na makataa yaliyokuwa yametangazwa na serikali mbalimbali kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya Corona.