NIGERIA-UFARANSA-SOKA

Victor Osimhen, ashinda tuzo ya Marc-Vivien Foé 2020

Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Lille ya Ufaransa Victor Osimhen kutoka Nigeria, ndio mshindi wa tuzo ya kila mwaka ya Marc-Vivien Foé inayotolewa na Idhaa ya RFI na Runinga ya France 24.

Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Lille ya Ufaransa Victor Osimhen (kushoto) kutoka Nigeria.
Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Lille ya Ufaransa Victor Osimhen (kushoto) kutoka Nigeria. AFP
Matangazo ya kibiashara

Tuzo hii, imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2009 kumtambua mchezaji kutoka barani Afrika aliyefanya vizuri katika ligi anayochezea kila mwaka.

Mwaka huu mshindi ni Victor Osimhen kutoka Nigeria anayechezea klabu ya Lille katika ligi kuu ya soka nchini Ufaransa ,alipatikana baada ya kupigiwa kura na wanahabari wa mchezo wa soka barani Afrika na nchini Ufaransa.

Osimhen mwenye umri wa miaka 21, msimu huu amekuwa mchezaji bira katika ligi ya Ufaransa kwa kuisaidia klabu yake kwa kufunga mabao 13 katika mechi 27.

Nafasi ya pili imechukuliwa na mshambuliaji kutoka Algeria, Islam Slimani, anayechezea klabu ya Monaco sawa na beki kutoka Morocco Yunis Abdelhamid, anayeichezea klabu ya Stade Rennais.

Tuzo hii imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2009 kumkumbuka Marc-Vivien Foé,mchezaji wa Cameroon aliyefariki dunia baada ya kuzimia uwanjani tarehe 26 mwezi Juni mwaka 2003 mjini Lyon, nchini Ufaransa.

Baadhi ya wachezaji wengine ambao wamewahi kushinda tuzo hii ni pamoja na Nicolas Pépé kutoka Cote d'Ivoire mwaka uliopita, Gervinho mara mbili miongoni mwa wengine.