PSG-SOKA-MICHEZO

Paris St-Germain yawaadhibu RB Leipzig mabao 3-0

Wachezaji wa Paris Saint-Germain kwenye mazoezi kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa.
Wachezaji wa Paris Saint-Germain kwenye mazoezi kabla ya mechi yao ya Ligi ya Mabingwa. Action Images via Reuters/Jason Cairnduff

Klabu ya soka kutoka nchini Ufaransa ya Paris St-Germain imtinga katika hatua ya fainali kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya, baada ya kuishinda RB Leipzig mabao 3-0 katika nusu fainali ya kusisimua iliyochezwa usiku wa kuamkia leo jijini Lisbon nchini Ureno.

Matangazo ya kibiashara

Mabao ya PSG yalitiwa kimyani na Marcos Marquinhos, Angel di Maria na  Juan Bernat.

PSG sasa inamsubiri mshindi wa nusu fainali ya pili leo, kati ya mabingwa mara tano wa taji hili Bayern Munich na Lyon ya Ufaransa, mechi itakayochezwa usiku wa leo katika uwanja wa Estádio José Alvalade jijini Lisbon.

Fainali itachezwa siku ya Jumapili, katika uwanja wa Estádio da Luz huko Lisbon Ureno.

Wakati huo huo fainali ya kuwania taji la Europa League itachezwa siku ya Ijumaa, kati ya Sevilla ya Uhispania na Inter Milan ya Italia.

Mechi hiyo itapigwa jijini Cologne nchini Ujerumani.

Hayo yanajiri wakati Ronald Koeman ameteuliwa kuwa kocha mpya wa klabu ya Barcelona.

Hili limethibtishwa na rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu.

Kocha Koeman, mwenye umri wa miaka 57, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya Uholanzi, anatarajiwa kuanza kazi baaadye wiki hii.

Na kuhusu ripoti kuwa, mshambuliaji wa muda mrefu na mwenye kipaji, Lionel Messi, anataka kuondoka katika klabu hiyo, rais huyo wa Barcelona amesema, Messi siku zote anataka kumalizia soka katika klabu hiyo na ana mkataba mpaka 2021.