CAF-SOKA

Coronavirus: Mkutano wa CAF kujadili maendeleo ya soka Afrika

Rais wa CAF Ahmad na mshauri wake nyota wa zamani Samuel Eto'o.
Rais wa CAF Ahmad na mshauri wake nyota wa zamani Samuel Eto'o. ISSOUF SANOGO / AFP

Rais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, Ahmad Ahmad yupo katika makao makuu ya Shirikisho hilo jijini Cairo, kwa maandalizi ya kuongoza kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika siku ya Alhamisi kwa njia ya video.

Matangazo ya kibiashara

Ajenda kubwa ya kikao hicho ni kutathmini maendeleo ya soka katika kipindi hiki ambacho bara la Afrika linaendelea kushuhudia janga la Corona, lakini pia, kitakuwa ni kikao cha kuangazia namna Mkutano Mkuu wa CAF utakavyofanyika mwezi Novemba.

Kikao hiki kitafanyika wiki hii wakati huu Shirikisho la soka nchini Misri likianza uchunguzi kuhusu kulitafuta kombe halisi la mashindani ya mataifa bingwa barani Afrika, lililoibwa wiki iliyopita.

Uchunguzi umeanzishwa na Shirikisho la soka la Misri FA (EFA) baada ya kubaini kuwa vikombe kadhaa vimepotea kutoka makao makuu yake mjini Cairo, likiwemo kombe asili la Mataifa ya Afrika.

Misri ilipokea zawadi ya kombe hilo iliposhinda michuano ya 2010, kwa kuwa ilikuwa imeshinda kombe la aina hiyo kwa mara ya tatu.

Maafisa nchini humo walivitafuta vikombe hivyo hivi karibuni tu, baada ya uamuzi wa kukarabati lango la EFA ili vikombe vingi ambavyo Misri imevipata viwekwe eneo la kuingia kwa ajili ya maonyesho.

Uvamizi wa EFA na mashabiki wenye jazba miaka saba iliyopita wakati wa ghasia mjini Cairo kwa sasa ni suala linaoangaliwa huku maafisa wakijaribu kubaini ni lini na ni vipi vikombe hivyo vilichukulia.