MICHEZO-RIADHA

Shura Kitata ashinda mbio za London Marathon, bingwa mtetezi Eliud Kipchoge aelemewa

Muethiopia Shura Kitata mwenye umri wa miaka 24 anapata ushindi wake mkubwa wa kwanza katika Mashindano ya London Marathon kwa kumuangusha Eliud Kipchoge.
Muethiopia Shura Kitata mwenye umri wa miaka 24 anapata ushindi wake mkubwa wa kwanza katika Mashindano ya London Marathon kwa kumuangusha Eliud Kipchoge. RICHARD HEATHCOTE / POOL / AFP

Shura Kitata wa Ethiopia ameshinda mashindanio ya riadha ya London Marathon mwaka 2020, na kumpiku bingwa wa mbio hizo mkenya Eliud Kipchoge aliyemaliza katika nafasi ya nane.

Matangazo ya kibiashara

Kitata, mwenye umri wa miaka 24, alitimka mbio hizo za kilomita 40 na kuibuka mshindi kwa muda wa saa 2 Dakika 5 na sekunde 41 akipata ushindani mkali kutoka kwa mkenya Vincent Kipchumba na Sisay Lemma kutoka Ethiopia waliomaliza katika nafasi za pili na tatu, kwa muda wa saa 2 Dakika 5 na sekunde 42 , huku Lemma akimaliza kwa muda wa saa 2 Dakika 5 na sekunde 45.

“Sijafurahishwa,” Alisema Kipchoge. “Sijui nini kilitokea. Nilitatizika baada ya kilomita 15 za mwisho, ambapo nilihisi sikio langu la kulia kuziba. Nilihisi maumivu kwenye nyonga na miguu.

“Nilianza mbio vizuri lakini tatizo hilo likatokea. Kuna barid kali lakini silaumu hali ya hewa.”

Bingwa mara nne wa mbio hizo za London Marathon, alikuwa amepewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi baada ya mpinzani wake mkuu Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia, kujitoa kushiriki, Ijumaa, kabla ya mashindano hayo kutokana na na jeraha.

Hata hivyo bingwa mwaka huu, amesema alipata mafunzo kutoka kwa Bekele, mbinu alizozitumia kuongeza kasi katika hatua ya mwisho ya mbio hizo na kumtoka mwiethopia mwenzake Lemma Sisay, na Mkenya Vincent Kipchumba.

“Nilijiandaa vizuri kwa mbio hizi. Kenenisa Bekele alinisaidia. Nafurahia ushindi huu.” Amesema Kitata

Kwa upende wa wanawake, Mkenya Brigid Kosgei anayeshikilia rekodi katika mbio hizo alitetea ubingwa wake kwa upande ya kina dada.

Kosgei, 26, alimtoka bingwa wa dunia Ruth Chepngetich baada ya kilomita 18, na kushinda mbio hizo kwa muda wa saa 2:18:58, dakika Tatu na sekunde Tatu mbele ya Mmarekani Sara Hall aliyemaliza wa Pili.

Kosgei ametia mfukoni Dola 30,000 (sawa na Euro 23,200) kutokana na ushindi wake.

“Nilijitahidi hadi mwisho licha ya hali mbaya ya hewa” Alisema mshindi huyo wa Chicago marathon.

“Hatukujiandaa vizuri kwa mbio hizi kutokana na janga la Corona. Nitajiweka tayari kwa matokeo bora zaidi mwakani.”

Mashindano hayo ya London marathon yalipangwa kufanyika mwezi Aprili lakini yakaratibiwa upya kutokana na janga la Corona. Mbio zilizoshirikisha wakimbiaji mashuhuri pekee katija mtaa wa St. James Park.