Patrice Motsepe aahidi makubwa iwapo atachaguliwa rais wa CAF

Patrice Motsepe anayegombea urais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF,  wakati akizungumza na wanahabari jijini Johannesburg siku ya Alhamisi Februari 25 2021
Patrice Motsepe anayegombea urais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF, wakati akizungumza na wanahabari jijini Johannesburg siku ya Alhamisi Februari 25 2021 Phill Magakoe AFP

Mgombea wa urais wa Shirikisho la soka barani Afrika CAF Bilionea Patrice Motsepe, kutoka Afrika Kusini, ameapa kuinua kiwango cha mchezo huo barani Afrika na kuleta umoja wa wadau wa mches wa kandanda iwapo atachaguliwa katika nafasi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Motsepe, ambaye ni mmoja wa wagombea wanne wa urais wa CAF, amezindua ilani au manifesto yake ya mambo 10 ambayo anaahidi kufanya iwapo atashinda nafasi hiyo.

Kila wakati nitakikisha kuwa, nawaunganisha waafrika kupitia mchezo wa soka, lakini pia nitahakikisha kuwa soka letu linakuwa na ushindani mkubwa Kimataifa.

 

Aidha, amekanusha madai kuwa  iwapo atachaguliwa, atahamisha makao makuu ya CAF kutoka jijini Cairo nchini Misri na kuyaleta jijini Johannesburg, huku akiongeza kuwa ni muhimu kutambua historia na mchango wa Misri katika maendeleo ya soka barani Afrika.

Mmiliki huyo wa klabu ya Mamelodi Sundowns, anatarajiwa kumenyana na wagombea wengine watatu, Jacques Anouma kutoka  Ivory Coast, Augustin Senghor kutoka Senegal na rais wa Shirikisho la soka nchini  Mauritania Ahmed Yahya.

Miongoni mwa viongozi wengine wa soka barani Afrika wanaomuunga mkono ni pamoja na rais wa soka nchini Nigeria Amaju Pinnick na Moucharafou Anjorin, rais wa soka nchini Benin.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 12 mwezi Machi nchini Morocco.