Ghana chini ya umri wa miaka 20, mabingwa wapya AFCON

Timu ya taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, wakishangilia baada ya kutwaa taji hilo dhidi ya Uganda. 06/03/2021
Timu ya taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, wakishangilia baada ya kutwaa taji hilo dhidi ya Uganda. 06/03/2021 © CAF Online

Timu ya taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20, wamefanikiwa kutwaa taji la michuano ya Mataifa ya Afrika mwishoni mwa juma wakati taifa lao likisherehekea miaka 64 ya Uhuru, baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 2 kwa bila dhidi ya Uganda, katika fainali iliyochezwa mjini Nouakchott.

Matangazo ya kibiashara

Nahodha wa Ghana, Daniel Afriyie, aliongoza kikosi chake vema ambapo alisherehekea kwa kipiga saluti akishuhudia timu yake ya taifa ikitwaa taji la 4 la michuano hiyo, na la kwanza tangu watwae taji hilo mwaka 2009.

Ushindi wa mabao mawili ulikuwa ni kama ule walioupata wakati wa fainali za mwaka 1978 wakati timu ya wakubwa ilipofanikiwa kutaa taji hilo.

Ghana walienda mapumziko wakiwa na goli moja kibindoni, ambapo Uganda itabidi wajilaumu wenyewe kwa kukosa nafasi kadhaa kwenye lango.

Mara ya mwisho kwa Ghana kushinda mashindano makubwa kama haya ilikuwa ni wakati wa vijana chini ya umri wa miaka 20 ya kombe la dunia, lakini ni bahati mbaya historia itashindwa kujirudia baada ya shirikisho la mpira duniani FIFA kuahirisha mashindano ya mwaka huu.

Ghana ilifika hatua ya mtoano baada ya kufuzu kama timu iliyopoteza mechi kwa kutoruhusu magoli mengi.

Kocha wa vijana wa Uganda, Morley Byekwaso, licha ya kupoteza katika mchezo wa Fainali, aliteuliwa kuwa kocha bora wa mashindano.

Rais wa Ghana, Nana Akufo Addo, ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Facebook kuwa;

Hongera kwa Black Satellites kwa kushinda taji la 4 la AFCON U20. Kiujumla ni ushindi mliostahili, na wameifanya Ghana kujivunia. Ushindi wa kipekee katika sherehe za miaka 64 ya uhuru.

Kwa ushindi wa mwaka 1993, 1999, 2009 na sasa 2021, Ghana inaungana na Misri kwa kuchukua mataji manne ya mashindano haya na wote wako nyuma kwa bingwa wa kihistoria wa michuano hii timu ya taifa ya Nigeria, yenye mataji 7.