Motsepe, rais mpya wa shirikisho la soka Afrika CAF

Patrice Motsepe, rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF
Patrice Motsepe, rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF REUTERS - SIPHIWE SIBEKO

Mkutano wa 43 wa shirikisho la soka barani Afrika CAF, umemchagua bilionea wa Afrika Kusini na mmiliki wa klabu ya Mamelod Sondowns, Patrice Motsepe, kuwa rais mpya wa shirikisho hilo, akichukua nafasi ya Ahmad Ahmad, ambaye anakibiliwa na tuhuma za ufisadi.

Matangazo ya kibiashara

Katika kongamano lililofanyika Rabat, nchini Morocco, wajumbe wa CAF walimchagua Motsepe, ambaye alikuwa mgombea pekee wa kiti hicho kufuatia ushawishi uliofanywa na shirikisho la soka la dunia FIFA.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Motsepe amesema;

Afrika inahitaji mshikamano wa pamoja na busara, lakini pia vipaji vya aina yake ambavyo vimekosekana kwa miaka kadhaa sasa.
Sote tukifanya kazi pamoja, soka la Afrika litashuhudia maendeleo na kukua kuliko ilivyowahi kushuhudiwa.

Bara la Afrika kwa miaka kadhaa sasa limeshuhudia hali duni ya soka, ambapo timu zote tano zilizoshiriki fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018, zilitupwa nje ya mashindano katika raundi ya kwanza, ikiwa ni hatua mbaya kushuhudiwa na timu za Afrika katika kipindi cha miaka 36.

Mwezi Novemba mwaka jana, Ahmad Ahmad, raia wa Madagascar, alikuwa rais wa kwanza wa CAF kufungiwa na FIFA kwa muda wa miaka 5 kutokana na masuala ya kiutawala, lakini adhabu hiyo ikapunguzwa hadi miaka miwili baada ya kukata rufaa katika mahakama ya kimataifa ya michezo CAS.

Rais wa shirikisho la soka Afrika CAF, anayemaliza muda wake, Ahmad Ahmad
Rais wa shirikisho la soka Afrika CAF, anayemaliza muda wake, Ahmad Ahmad france24.com

Wiki kadhaa nyuma, Motsepe, Jacques Anouma, rais wa shirikisho la soka la Ivory Coast, Mmauritania, Ahmed Yahya na Msenegal Augustin Seghor, walikuwa wakivutana kuwania kiti hicho kabla ya FIFA kuingilia kati na kupendekeza Motsepe achaguliwe.

Seghor na Yahya hata hivyo walipewa nafasi za makamu wa kwanza na wapili wa rais wa shirikisho la soka Afrika CAF.

Anouma, ambaye awali alikosoa uamuzi wa FIFA kuingilia kati, ameteuliwa kuwa mshauri maalumu wa Motsepe.

Licha ya baadhi ya nchi wanachala kukosoa kitendo cha FIFA kuingilia kati mchakato wa uchaguzi wa CAF, rais wa FIFA, Gianni Infantino, alikanusha madai hayo.

Changamoto takribani sita zitakuwa zikimkabili Motsepe, ikiwemo masuala ya rushwa, utawal, haki za matangazo ya televisheni, mawasiliano na hasa tovuti ya CAF pamoja na suala la waamuzi ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa vitendo vya Rushwa.