Viongozi wa soka wakutana nchini Morocco kumwidhinisha Motsepe kuwa rais mpya wa CAF
Imechapishwa:
Viongozi wa mchezo wa soka kutoka mataifa 54 ya bara Afrika, wanakutana mjini Rabat nchini Morocco kwenye mkutano wao mkuu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu mchezo huo.
Kikubwa ni kumwidhinisha Patrice Motsepe kuwa rais mpya wa Shirikisho la soka barani Afrika.
Bilionea huyo raia wa Afrika Kusini, na mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns, hana mpinzani baada ya wapinzani wake watatu Augustin Senghor, Jacques Anouma na Ahmed Yahya kujiondoa siku chache kuelekea kwenye uchaguzi huo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Shirkisho la soka duniani FIFA, kupendekeza kuwa wagombea hao wamwachie Motsepe nafasi hiyo huku Senghor, Yahya wakipendekezwa kuwa manaibu rais wa CAF na Anouma kuwa mshauri wao mkuu.
Motsepe anachukua nafasi ya Ahmad Ahmad ambaye wakati wa utawala wake, alifungiwa kutojihusisha na masuala ya soka na FIFA kwa miaka mitano baada ya kupatikana na kosa la kukiuka maadili ya uongozi wa soka.
Hata hivyo, Mahakama ya Kimataifa kutatua mizozo ya michezo ilimpunguzia Ahmad raia wa Madagascar adhabu hiyo na kumfungia sasa kwa miaka miwili, baada ya kusikiliza rufaa yake.
Historia ya viongozi wa soka barani Afrika:
1957 Abdel Aziz Abdallah Salem (Misri)
1958 Abdel Aziz Moustafa (Misri)
1968 Abdel Halim Muhammad (Sudan)
1972 Yidnekatchew Tessema (Ethiopia)
1987 Abdel Halim Muhammad (Sudan)
1988 Issa Hayatou (Cameroon)
2017 Ahmad Ahmad (Madagascar)
Kumbuka: Constant Omari Selemani kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekuwa akikaimu urais wa CAF kwa siku 67, tangu Novemba 23, 2020 baada ya Ahmad kufungiwa na FIFA.