Motsepe: AFCON kuendelea kuchezwa kila baada ya miaka 2

Rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF, Dr Patrice Motsepe
Rais wa shirikisho la soka barani Afrika, CAF, Dr Patrice Motsepe © CafOnline Media

Rais wa shirikisho la soka barani Afrika CAF, Dr Patrice Motsepe, amesema mfumo wa sasa wa fainali za kombe la mataifa ya Afrika, AFCON, utasalia kama ulivyo.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumzia kwa mara ya kwanza mikakati yake ya kulibadili shirikisho hilo, Motsepe amesema mfumo wa sasa wa kila miaka 2 kufanyika kwa mashindano ya AFCON, utabaki kama ulivyo.

"AFCON, ilivyo sasa, lazima iendelee kufanyika kila baada ya miaka 2, hata hivyo suala hili bado halijafungwa, majadiliano na wadau yataendelea kufanyika."

Awali wakati wa mkutano wa 43 wa CAF, Motsepe ambaye alichaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho hilo, aliapa kuzitembelea nchi zote wanachama 54 wa CAF katika kipindi cha miezi 9 ijayo.

Dr Motsepe, pia alieleza mkakati wake wa kuwa na mikutano ya mara kwa mara ya nchi wanachama kama sehemu ya kuboresha mfumo shirikishi.

"Nitafanya mikutano miwili zaidi mwaka huu na marais wa vyama vya soka na tutajadiliana mikakati ya dharura,"
Rais mpya wa CAF, Patrice Mptsepe, akizungumza juma lililopita baada ya kuchaguliwa
Rais mpya wa CAF, Patrice Mptsepe, akizungumza juma lililopita baada ya kuchaguliwa © CafOnline Media

Akiwa na uzoefu mkubwa katika biashara, rais Motsepe aliongeza kuwa:

"Sitakubali kuwa rais wa taasisi ambaye katika kipindi cha miaka 4, sitakuwa nimefanya chochote kinachoonekana na cha kimaendeleo, sitaruhusu hilo."

"Tuache kuwa watu wa matumaini. Ni muhimu kutambua madhaifu yetu na makosa, Na tutayarekebisha."