FIFA yashusha rungu jingine kwa Sepp Blatter na Jerome Valcke

Aliyekuwa rais wa FIFA, Sepp Blatter, hii ilikuwa ni picha ya mwaka 2015
Aliyekuwa rais wa FIFA, Sepp Blatter, hii ilikuwa ni picha ya mwaka 2015 FABRICE COFFRINI AFP/File

Shirikisho la soka duniani FIFA, limetangaza adhabu mpya dhidi ya aliyekuwa rais wa shirikisho hilo, Sepp Blatter, ambapo sasa atatumikia adhabu nyingine ya miaka 6 na miezi 8 ya kutojihusisha na masuala ya soka hadi mwaka 2028.

Matangazo ya kibiashara

Aliyewahi kuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo, Jerome Valcke, nae amepewa adhabu inayofanana na Blatter ambapo pia ametakiwa kulipa faini ya euro laki 7 na elfu 80.

Kwa mujibu wa FIFA, adhabu zao zinatokana na makosa ya ukiukaji maadili ya kiutendaji.

Adhabu hizi mpya dhidi ya viongozi hawa, zitaanza kutekelezwa baada ya kumalizika kwa adhabu za sasa wanazotumikia kati ya mwezi Octoba 2021 na Octoba 2025.

Taarifa ya FIFA imesema;

Uchunguzi dhidi ya Blatter na Valcke, ulihusu tuhuma kadhaa na hasa malipo ya ziada yaliyohusiana na mashindano ya kimataifa yaliyoandaliwa na FIFA na kufanywa kwa viongozi hawa na viongozi wengine wa shirikisho hilo, marekebisho ya sheria kadhaa za manunuzi na kuongezwa muda wa mikataba, pamoja na malipo binafsi ya mawakili kwa kesi iliyomuhusu Valcke.

Katika uchunguzi wake, FIFA ilibaini kuwa Blatter, alikubaliana kupewa malipo kinyume cha sheria ya kiasi cha Franga za Uswis milioni 23 kati ya mwaka 2010 na 2014.

Uchunguzi ulibaini pia Bmatter, Valcke pamoja na aliyekuwa rais wa shirikisho la soka la Argentina, Julio Grondona na aliyekuwa mkurugenzi wa fedha wa FIFA, Markus Kattner, walijitengenezea utaratibu uliofanya wapokee malipô kinyume cha sheria za maadili za FIFA.

Awali Blatter alikuwa amefungiwa na FIFA kwa miaka 8 kutojihusisha na soka lakini baadae adhabu hiyo ilipunguzwa hadi kufikia miaka 6, ambapo alidaiwa kufanya malipo ya paundi milioni 1.3 kwa aliyekuwa rais wa shirikisho la soka la Ulaya, Michel Platini.

Valcke yeye adhabu yake ya awali ilikuwa ni kutojihusisha na soka kwa miaka 12 lakini baadae ilipunguzwa hadi kufikia miaka 10.