JAPAN-MICHEZO

Tokyo 2021: Mabondia wa Afrika waanza vizuri, wapata medali ya kwanza Taekwondo

Bondia kutoka Cameroon Albert Menue Ayissi (kushoto) akimenyana na bondia kutoka Eswatini Thabiso Dlamini, Julai 24, 2021.
Bondia kutoka Cameroon Albert Menue Ayissi (kushoto) akimenyana na bondia kutoka Eswatini Thabiso Dlamini, Julai 24, 2021. REUTERS - FRANK FRANKLIN II

Baada ya sherehe ya ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya Tokyo, wanariadha kutoka Afrika wamefanya vizuri Jumamosi hii katika mashindano hayo yanayoendelea katika mji mkuu wa Japan, Tokyo. Katika ndondi, wamefanya vizuri kwa kupata ushindi.

Matangazo ya kibiashara

Mtunisia Mohamed Khalil Jendoubi amepata medali ya fedha katika mchezo wa Taekwondo. Lakini katika michezo mingine, hawajafua dafu.

Ndondi

Mcameroon Albert Menue Ayissi amefanya vizuri katika mzunguko wa 8 kwa wale walio chini ya kilo 69 (katikati ya uzito). Bondia huyo mwenye umri wa miaka 22 ameshinda pambano lake dhidi ya Thabiso Dlamini kutoka Eswatini baada ya kumlainisha kwa makonde. Siku ya Jumanne atamenyana na bondia kutoka Ireland Aidan Walsh.

Merven Clair kutoka Mauritius, aliyeshinda medali ya Dhahabu katika Michezo ya Afrika ya 2019, na Mzambia Stephen Zimba, pia wametinga katika mzunguko unaofuata kufuatia ushindi wao kwa pointi, dhidi ya mchezaji kutoka Canada Wyatt Sanford na Marion Faustino Ah Tong.

Mersen Clair atamenyana na Mjordan Zeyad Eishaih Hussein Eashash siku ya Jumanne, wakati Stephen Zimba atapepetana na na Mrusi Andrei Zamkovoi.