AFCON 2021-CAMEROON-SOKA

AFCON: Ghana wakerwa na sare waliyopata dhidi ya Gabon

Nahodha wa timu ya soka ya Ghana Andre Ayew,  ameiita Gabon timu ndogo baada ya timu hiyo kutoka nyuma katika dakika za lala salama  na kusawazisha bao 1 walilokuwa wamefungwa  katika kipindi cha kwanza cha michuano ya kuwania taji la mataifa ya Afrika, Ijumaa usiku, mechi  iliyokamilika kwa sare ya  bao 1-1.

Ghana ikichuana na Gabon, mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1.
Ghana ikichuana na Gabon, mechi hiyo iliisha kwa sare ya bao 1-1. Kenzo Tribouillard AFP
Matangazo ya kibiashara

Gabon ilipata bao la kusawazisha dakika ya 88 baada ya mchezaji wake Jim Allevinah kuvurumisha kombora kuelekea lango la Ghana, bao ambalo liliwakera wachezaji wa Black Stars waliokuwa wanalalamikia  kufungwa wakati mchezaji wao Daniel-Kofi Kyereh akiwa ameangushwa chini.

“Sisi tuliutoa mpira nje, bada ya mchezaji wetu kuangushwa, na ningekuwa kitendo cha uungwana kuturejeshea mpira, lakini walitumia fursa hiyo kufunga, ndivyo timu ndogo zinavyofanya,” alisema Ayew.

Baada ya mchezo huo kufika tamati wachezaji wa timu zote walianza kurushiana makonde na mchezaji wa Ghana Benjamin Tetteh kuoneshwa kadi nyekundu kwa kumpiga mchezaji wa timu pinzani.

Gabon ilicheza mchuano huo bila ya mshambuliaji wake wa kutegemewa Pierre-Emerick Aubameyang na kiungo wa Kati Mario Lemina walioambukizwa virusi vya Covid 19.

Matokeo hayo katika kundi C, yalikuja baada ya mshindani mwingine, Morocco kufuzu katika hatua ya mwondoano baada ya kushinda mechi zake mbili za kundi hilo na inaongoza kwa alama sita.

Ghana baada ya mechi mbili, wana alama mpja, Gabon ni wa pili katika kundi hilo kwa alama nne, Morocco wana alama sita, baada ya mechi ya pili kuishinda Comoros wanaoshiriki kwa mara ya kwanza, mabao 2-0.

Mechi za mwisho za kundi C- Januari 18 2022

Gabon vs Morocco

Ghana vs Comoros

Matokeo ya mechi za awali.

Morocco 1-0 Ghana

Comoros 0-1 Gabon

Morocco 2-0 Comoros

Gabon 1-1 Ghana