BRAZILI-SIASA-UCHUMI

Dilma Rousseff: "vita ndio bado vinaanza"

Rais wa Brazil Dilma Rousseff, Machi 22, 2016 Brasilia.
Rais wa Brazil Dilma Rousseff, Machi 22, 2016 Brasilia. REUTERS/Adriano Machado

Rais wa Brazil amejibu Jumatatu Aprili 18 kuhusu uamuzi wa Wabunge waliopiga kura katika neema ya kumtimua mamlakani. Rais Dilma Rousseff amesema "kuchukizwa" na uamuzi huo wa Wabunge, huku akiahidi kuendelea na mapambano dhidi ya utaratibu huo. Kwa sasa hatma ya Rais Rousseff iko mikono mwa Baraza la seneti.

Matangazo ya kibiashara

Dilma Rousseff ana "hasira". Baada ya uamuzi wa Wabunge katika neema ya kumng'oa madarakani, uamuzi uliopasishwa katika kikao cha kihistoria cha Jumapili usiku. Hata hivyo majibu ya rais wa Brazil yalikua yakitarajiwa.

Rais Rousseff, ambaye alionekana akiwa na hasira, ametangaza uamuzi wake: sintokubali kuachia ngazi. "Nitapambana, pambano bado linaendelea," amesema Rais wa Brazil Jumatatu hii Aprili 18 katika mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya rais.

Dilma Rousseff, ambaye amerejelea kauli yake ya mwanzo kwamba hajafanya "uhalifu wowote" ameonyesha kuwa yuko tayari kupambana, ingawa kwa undani amejeruhiwa na utaratibu huo unaolenga kumtimua mamlakani, ambao anauchukulia kama "dhulma".

Alimnyooshea kidole cha lawama makamu wake, Michel Temer, akimshtumu kupanga njama za kumng'atua madarakani.

"Mimi, nilichaguliwa kwa kura milioni 54. Uamuzi wa Wabunge wa kukubali kuanzisha utaratibu wa kunitimua mamlakani, umeniudhi. Lakini cha muhimu ni kwamba hakuna mashtaka dhidi yangu ya ubadhirifu wa fedha za umma au utajiri haramu, na sijashtumiwa kuwa na akaunti za siri zilizofichwa nje ya nchi. Ni kwa sababu hio naona kwamba sitendewi haki, na nafanyiwa dhulma ya kutisha, kwa kuwa yule ambaye anajihusisha na vitendo haramu, ambaye ana akaunti za benki za siri, ni mtu huyo huyo ambaye aliongoza kikao cha Bunge," Rais Dilma Rousseff amesema.

Rais Rousseff amesema kuwa "hana mpango sasa" kwa ajili ya uchaguzi wa haraka.

Jumapili jioni, Wabunge walipiga kura ya kutokua na imani na Rais Dilma Rousseff na kuomba ang'atuliwe madarakani. Rais Dilma Rousseff, kutoka mrengo wa kushoto, Madarakani tangu mwaka 2010, anashtumiwa kutumia fedha za umma wakati wa kampeni zake za siasa mwaka 2014.