KENYA-MAANDAMANO

Maandamano dhidi ya Tume ya Uchaguzi yavunjwa Nairobi

Mji wa Nairobi umekumbwa JUmatatu hii Mei 16 na maandamano ya wafuasi wa upinzani wakiomba kuvunjwa kwa Tume ya Uchaguzi.
Mji wa Nairobi umekumbwa JUmatatu hii Mei 16 na maandamano ya wafuasi wa upinzani wakiomba kuvunjwa kwa Tume ya Uchaguzi. Reuters/Noor Khamis/File Photo

Polisi ya Kenya imetumia mabomu ya machozi na kurusha maji kwa kuwatawanya mamia ya waandamanaji ambao walimiminika Jumatatu hii mitaani wakitaka kuvunjwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), wakidai kwamba inaegemea upande fulani, shirika la habari la Reuters limearifu.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni mara ya tatu katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja maandamano ya kutaka kuvunjwa kwa taasisi hiyo inayotakiwa kuhakikisha uhuru wa uchaguzi yanafanyika na kusababishamakabiliano kati ya waandamanaji na polisi.

Waandamanaji walirusha mawe dhidi ya polisi. "Kwa uchaguzi huru na wa haki, IEBC inapaswa kuondoka," hayo ni maneneo ambayo yalikua yameandikwa kwenye bango moja lililokua limebebelewa na mmoja wa waandamanaji.

Maandamano kama haya yamefanyika pia mjini Kisumu na katika ngome zingine za muungano wa upinzani CORD huku ripoti zikisema baadhi ya waandamanaji wamejeruhiwa baada ya kupigwa na maafisa wa polisi.

Uchaguzi wa rais na ule wa wabunge umepangwa kufanyika mwezi Agosti 2017. Lakini wanasiasa tayari wameanza kampeni katika nchi ambapo raia wengi bado wana kumbukumbu ya ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Watu 1,200 waliuawa katika machafuko hayo ambapo migawanyiko ya kikabila ilichochewa na mivutano ya kisiasa.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2013 pia yalizua shutma za udanganyifu kwa upinzani.

Hata hivyo viongozi wa muungano wa Cord nchini Kenya wameapa kuendelea na maandamano ya amani kudai kujiuzulu kwa makamishna wa uchaguzi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao na marekebisho ya tume ya uchaguzi IEBC.

Maandamano hayo yametangazwa kufanyika Jumatatu kila wiki hadi viongozi wa tume hiyo waondoke ofisini.

Upinzani unadai kwamba makamishna hao ni mafisadi na wanapendelea serikali madai ambayo makamishna wamekanusha.

Serikali imewataka upinzani kuacha maandamano na kufuata katiba ili kuwaondoa makamishna hao.

Rais Uhuru Kenyatta, ambaye anapaswa kuwania muhula wa pili mwaka ujao, ametoa wito kwa wapinzani wake kutoingia mitaani.