MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA

Hillary Clinton ashindwa kumuangusha Bernie Sanders

Bernie Sanders aendelea kutimuana vumbi na Hillary Clinton, wote kutoka chama cha Democratic, katika kura za mchujo
Bernie Sanders aendelea kutimuana vumbi na Hillary Clinton, wote kutoka chama cha Democratic, katika kura za mchujo REUTERS/Jim Young

Baada ya kampeni ngumu, mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton amedai ushindi mdogo Jumanne hii katika jimbo la Kentucky katika kura za mchujo. Lakini Bernie Sanders, ambaye ameibuka mshindi katika jimbo la Oregon, ameahidi kubaki katika mbio za urais katika chama cha Democratic hadi mwisho.

Matangazo ya kibiashara

Afisa anayesimamia uchaguzi katika jimbo la Kentucky, Alison Lundergan Grimes, ametangaza kwenye runinga ya CNN kwamba Hillary Clinton ameshinda uchaguzi katika jimbo hilo.

"Tumeshinda uchaguzi katika jimbo la Kentucky!" Hillary Clinton ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter.

Kwa mujibu wa matokeo kwa jumla ya 99.9% ya vituo vya kupigia kura, Hillary Clinton amepata 46.8% ya kura dhidi ya 46.3% ya kura alizopata Seneta kutoka Vermont, sawa na chini ya kura 2,000 kwa jumla ya zaidi ya kura 450,000.

Lakini Bernie Sanders amemshinda kirahisi Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekanii, katika jimbo la Oregon, katika pwani ya Pasifiki, kwa 53% ya kura kwa mujibu wa matokeo ya awali.

Chama cha Republican kimeendesha zoezi la uchaguzi wa mchujo katika jimbo la Oregon pekee. Donald Trump, mgombea pekee katika mbio hizo, ingawa majina ya washindani wake wa zamani yamebakia kwenye kadi za kura.