Hillary Clinton akaribisha ushindi wake
Imechapishwa:
Mgombea wa urais nchini Marekani anayewania kuteuliwa na chama chake cha Democratic, Hillary Clinton, amepongeza ushindi alioupata usiku wa kuamkia leo, na kudai kuwa ni wakihistoria hasa kwa wanawake wa taifa hilo.
Clinton amemuacha kwa mbali mpinzani wake wa karibu, Barnie Sanders ambaye amempongeza kwa kuendelea kumpa changamoto kwenye kampeni zake, lakini akasisitiza umuhimu wa kuungana ili kumshinda Donald Trump ambaye amesema hana uwezo wa kuliongoza taifa hilo.
Kwa upande wake mgombea wa Republican, Donald Trump ameendelea kumkashifu Hillary Clinton, akidai kuwa ni mlaji wa rushwa na aliyetumia barua pepe binafsi kuficha uhalifu aliokuwa anaufanya wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, na kwamba Jumatatu ya wiki Ijayo atatoa hotuba ya aina yake itakayoweka wazi udhaifu wa Clinton.
Kwa ushindi huu, inamaanisha kuwa tayari Hillary Clinton amepata idadi ya wajumbe wanaohitajika kumuidhinisha kupeperusha bendera ya chama chake, ambapo ni mara tatu ya idadi ya wajumbe alio nao mpinzani wake Barnie Sanders anayesubiriwa kutangaza kujiondoa kwenye mbio wakati wowote kuanzia sasa.