TANZANIA-KENYA-SABA SABA

Siku ya Saba Saba kwa Kenya na Tanzania

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati walipotembelea maonesho ya kimataifa ya Saba saba nchini Tanzania, hivi karibuni.
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati walipotembelea maonesho ya kimataifa ya Saba saba nchini Tanzania, hivi karibuni. Ikulu/Tanzania

Je, wajua kuwa siku ya Saba Saba ni siku ya kihistoria katika nchi ya Kenya na Tanzania? Nchini Tanzania, siku kama ya leo mwaka mwaka 1954 chama cha Tanganyika African Nation Union kiliundwa, wakati taifa hilo lilifahamika kwa jina la Tanganyika.

Matangazo ya kibiashara

Wanasiasa wa wakati huo wakiongozwa na Baba wa Taifa wa hilo Julius Nyerere walitumia chama hicho kujikomboa kutoka kwa wakoloni kuelekea kupata Uhuru mwaka 1961, na baadaye kuvunjwa mwaka 1977.

Hata hivyo, siku hii nchini Tanzania haikumbukwi tena kama siku ya kisiasa bali ni siku ya mapumziko kuadhimisha kilele cha maonyesho ya kimataifa ya kibiashara yaliyopewa jina Saba Saba.

Maonesho haya yaliadhimishwa mara ya kwanza mwaka 1963 na huwakutanisha wafanyibiashara mbalimbali kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwingineko duniani, kuonesha bidhaa mbalimbali wanayouza au vifaa wanavyotenegeza.

Maadhimisho ya mwaka huu yalifunguliwa rasmi na rais wa Rwanda Paul Kagame.

Nchini Kenya, siku ya Saba Saba sio siku ya mapumziko ya kitaifa lakini wanaharakati na wanasiasa wanakumbuka siku hii mwaka 1990 walipofanya mkutano wa kihistoria katika uwanja wa Kamkunji jijini Nairobi, kushinikiza mabadiliko ya Katiba mpya kuruhusu kuwepo kwa vyama vingi.

Serikali ya wakati huo ya chama kimoja cha KANU ikiongozwa na Rais Daniel Torotich Arap Moi, ilikataa kutoa kibali cha kufanyika kwa mkutano huo lakini wanaharakati na wanasiasa hao wakiongozwa na Charles Rubia, Martin Shikuku, Raila Odinga, Gitobu Imanyara, Jaramogi Oginga Odinga na wengine waliendelea na mkutano huo kwa nguvu.

Vurugu zilizuka jijini Nairobi kwa siku nne na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20 kupoteza maisha na zaidi ya wengine 1,000 kukamatwa.

Baada ya Shinikizo hizo, rais wa wakati huo Daniel Arap Moi alikubali kuwepo kwa vyama vingi.

Hii ndio tofauti kati ya kumbukuka siku ya Saba Saba nchini Tanzania na Kenya.