GABON-UCHAGUZI

Jean Ping awasilisha madai yake katika Mahakama ya Katiba

Mpinzani mkuu nchini Gabon, Jean Ping, Agosti 27, 2016 mjini Libreville.
Mpinzani mkuu nchini Gabon, Jean Ping, Agosti 27, 2016 mjini Libreville. STEVE JORDAN / AFP

Mpinzani mkuu nchini Gabon, Jean Ping, hatimaye amewasilisha madai yake katika mahakama ya Katiba na kuomba kuhesabiwa upya kura za uchaguzi. Mwenyekiti huyo wa zamani wa Umoja wa Afrika, anaendelea kupinga ushindi wa Ali Bongo Ondimba uliyotangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Tume ya Uchaguzi.

Matangazo ya kibiashara

Sheria ya Gabon inabaini kwamba katika hali ya mzozo wa uchaguzi, wale ambao hawakuridhishwa na matokeo ya uchaguzi, wanatakiwa kuwasilisha madai yao mbele ya mahakama ya juu nchini.

Upinzani ulikua umebaki na muda wa kuwasilisha madai yake hadi Alhamisi hii jioni.

Wengi miongoni mwa wafuasi wa upinzani wanaamini kwamba Mahakama ya Katiba ni chombo kinachoendesha shughuli zake kwa maslahi ya Rais Ali Bongo.

Upinzani hauna imani na Mahakama ya Katiba, kwani unaamini kwamba chombo hiki kimekua kikishawishiwa na utawala. Kambi ya Jean Ping unashtumu kwanza muundo wa Mahakama ya Katiba, kwani majaji wake tisa wanachaguliwa na Rais wa Baraza la Seneti na rais wa nchi mwenyewe. Mkuu wa Mahakama anachaguliwa kutoka kwa majaji wa Mahakama hiyo walioteuliwa na Rais Bongo.

Licha ya hali ya utulivu kurejea katika maeneo mbalimbali nchini Gabon, mvutano wa kisiasa bado unaendelea, na hofu ya kutokea kwa machafuko zaidi imeendelea kutanda katika baadhi ya miji.

Hayo yakijiri Umoja wa Afrika umeahirisha kutuma ujumbe wake utakaohusika na kuchangia kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Gabon. Umoja wa Afrika haujaleza tarehe nyingine ambapo ujumbe huo utatumwa, Waziri wa mambo ya Nje wa Gabon, Emmanuel Isozet Ngondet, ametangaza Alhamisi hii Septemba 8.