BURKINA FASO-MAWASILIANO

Mtandao wa simu wavurugika kwa mgomo nchini Burkina Faso

Nchini Burkina Faso, mtandao wa simu umevurugika kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa shirika la umma la Mawasiliano (Onatel).
Nchini Burkina Faso, mtandao wa simu umevurugika kutokana na mgomo wa wafanyakazi wa shirika la umma la Mawasiliano (Onatel). Getty Images/Per-Anders Pettersson

Raia nchini Burkina Faso wamekua na hasira kutokana na kukosa mawasiliano kupitia simu. Wafanyakazi wa shirika la umma la Mawasiliano (Onatel) wamo katika mgomo kwa zaidi ya wiki moja sasa. Kutokana na hali hiyo mawasiliano yamevurugika kwenye mtandao wa simu za mkononi na kadi huduma za simu hazipatikani kiurahisi.

Matangazo ya kibiashara

Wafanyakazi wanashutumu usimamizi wa kampuni ya mawasiliano ya simu na wanaomba mishahara iongezwe na mazingira ya kazi yaboreshwe. "Kuna ukosefu wa rasilimali katika ofisi zetu, katika viwanda vyetu katika vituo vya matengenezo na uzalishaji, ambavyo vinatia ugumu katika suala la huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukarabati baadhi ya mbambo," amesema Souleymane Sow, katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya simu katika ngazi ya taifa.

Matokeo ya mgomo: matatizo katika kuwasiliana kwenye mitandao na misukosuko au kusumbuliwa kwa upatikanaji wa Intaneti katika miji kadhaa.

Raia waghadhabishwa

Kadi za salio zimekua nadra kwenye soko na hali hiyo imewaghadhabisha wateja mbalimbali wanaonufaika na huduma hiyo. Ukosefu wa mawasiliano nchini Burkina Faso umesababisha shughuli nyingi kuzorota.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wateja wametishia kuandamana hadi kwenye makao makuu ya kampuni ya mawasiliano ya simu. Wengine wameamua tu kununua kadi mpya za simu kawenye makumpuni mengine. "Ndani ya siku tatu, kama hakuna ufumbuzi, tutaingia mitaani, " amsema mmoja wa wakazi mji wa Ouagadougou.

Hivi karibuni wawakilishi wa wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano walipokelewa na Waziri Mkuu, lakini mawasiliano bado yanasumbua nchini Burkina Faso.