Serikali mpya yaundwa nchini Gabon

Nchini Gabon, Waziri Mkuu mpya Franck Emmanuel Issoze-Ngondet ametangaza serikali yake mpya. Serikali hiyo ina wajumbe 40, idadi sawa na ile ya serikali iliyotangulia. Watu wengi wamekua wakijiulizi kama kweli serikali hii mpya ni ya umoja kama alivyoahidi Rais Ali Bongo.

Waziri Mkuu mpya wa Gabon Emmanuel Issoze-Ngondet aunda serikali yake yenye wajumbe 40.
Waziri Mkuu mpya wa Gabon Emmanuel Issoze-Ngondet aunda serikali yake yenye wajumbe 40. STEVE JORDAN / AFP
Matangazo ya kibiashara

Namba mbili katika serikali hii ni Bruno Ben Moubamba, mwanasiasa wa upinzani , ambaye bado kijana, aliyechukua nafasi ya tatu katika uchaguzi wa rais wa Agosti 27. Ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu anayehusika na Nyumba na Makazi. Hata hivyo, hakuna mwanasiasa wa upinzani anayemuunga mkono Jean Ping ambaye ameteuliwa katika serikali hii mpya. Jean Ping, ambaye bado anadai kuwa ni rais aliyechaguliwa ameendelea na msimamo wake na kuwataka wafuasi wake kuendelea kupinga uamuzi wa Mahakama ya Katiba wa kuidhinisha matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi iliyomtangaza Ali Bongo kama mshindi wa uchaguzi huo.

Serikali ina 30% ya wanawake. Na ilibadilika hadi 50%. Washirika wa karibu wa Ali Bongo wanashikilia nyadhifa muhimu. Katibu Mkuu wa Ofisi ya rais wa Jamhuri ni Etienne Massard Makaga, ambaye ataendesha majukumu yake na yale ya Waziri wa Ulinzi. Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Pachomius Moubelet Boubeya, amepandishwa cheo na kuwa Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Mambo ya Nje.

Alain Claude Bilie By Nze pia amefanikiwa kupata nafasi katika serikali hii mpya. Ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi mwenye dhamana ya Uchumi, Mawasiliano na Utamaduni na Msemaji wa Serikali.

"Hii ni serikali ambayo inaundwa na wanaume na wanawake kutoka vyama vya upinzani, vyama vya kiraia, lakini pia vyama vinavyomuunga mkono Ali Bongo. Hii ni serikali yenye lengo la kuliendeleza taifa na kutoa fursa sawa, lakini pia kuanzisha mazungumzo na wadau wote muhimu wa taifa hili, " amesema Bw By Nze. Hii ni Serikali ilio wazi, lakini si serikali ya umoja wa kitaifa. "Hapa tupo katika hatua ya ufunguzi na baadaye taangalia jinsi ya kushirikisha upinzani zaidi au vyama vinavyounga mkono serikali, " ameongeza Bw By Nze.