DRC-SIASA

DRC: Rais Kabila aahidi uchaguzi wa amani, huru na haki

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Oktoba mwaka jana katika mji wa Beni.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Oktoba mwaka jana katika mji wa Beni. © AFP PHOTO/ALAIN WANDIMOYI

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC ameahidi kuwa serikali yake inaandaa mazingira mazuri ili uchaguzi ufanyike kwa amani kupitia mazungumzo ya kitaifa yanayoendelea nchini humo.Rais Joseph Kabila ameyasema hayo Jumanne wiki hii wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania na kuongeza kuwa uchaguzi huo utakua huru na wa haki licha ya nchi hiyo ya changamoto ya kiusalama Mashariki mwa nchi hiyo.  

Matangazo ya kibiashara

'Uchaguzi utafanyika mwaka huu au siku nyingine'. Alisema Rais Joseph Kabila Kabange na kuongeza kuwa 'yote yatategemea mazungumzo yanayoendelea mjini Kinshasa.'

Joseph Kabila amesema 'itakua bora kuandaa uchaguzi kwa muda muafaka', akibaini hasa kwamba wapiga kura hadi milioni kumi hawajajiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na wanaweza kujihusisha na vurugu kama watakua hawakushiriki uchaguzi.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amepuuzilia mbali madai ya kuwepo mvutano wa kisiasa nchini mwake.

Hata hivyo Rais Kabila amevinyooshea kidole cha lawama vyombo vya habari akisema vinapotosha halisi iliyopo nchini humo.

Tume ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo, CENI, mwishoni mwa juma lililopita, ilisema inapanga kuomba kusogezwa mbele kwa tarehe ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, sasa ufanyike mwenzi November mwaka 2018.

Tangazo la tume ya uchaguzi nchini DRC, limekuja wakati huu upinzani nchini humo ukihofia kuwa huenda rais Joseph Kabila akasalia madarakani wakati muda wake utakua umemalizika ifikapo mwezi Desemba.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo, Corneile Naanga, amesema kuwa wameomba uchaguzi huo usogezwe mbele ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa maandalizi mazuri zaidi yatakayopelekea kuwa na uchaguzi ulio huru na haki.

Hivi karibuni zaidi ya watu 50 waliripotiwa kuuawa na polisi kutokana na maandamano ya upinzani dhidi ya rais Kabila.

Hayo yanajiri wakati ambapo Ufaransa, kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje Jean-Marc Ayrault, kwenye runinga ya TV5 Monde Jumatatu wiki hii, alimtaka Rais wa sasa wa DR Congo kuheshimu Katiba na kutowania muhula mwengine.

Wakati huo huo Ufaransa imetishia kuichukulia vikwazo nchi hiyo. Ayrault amesema: ''Rais Kabila lazima aonyeshe mfano mwema. Ni lazima aheshimu katiba. Iwapo vikwazo vitahitajika tutaamua kuvitekeleza. Nataka watu waelewe; Watu waliopo katika mamlaka DRC ni lazima wawajibike. Iwapo wanahitaji amani nchini mwao, iwapo wanajali hali ya watu wao ,ni lazima wafuate katiba''.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kwa upande wake, imesema Ufaransa inachochea maasi dhidi ya serikali nchini humo.

Waziri wa Mawasiliano Lambert Mende ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Ufaransa 'inacheza mchezo hatari'.