SYRIA-USALAMA-SIASA

Washington na Moscow kujaribu tena kukutana kuhusu Syria

Sergei Lavrov (kushoto), Waziri wa mambo ya Nje wa Urusi atakutana na mwenzake wa Marekani John Kerry mjini Lausanne siku ya Jumamosi Oktoba 15.
Sergei Lavrov (kushoto), Waziri wa mambo ya Nje wa Urusi atakutana na mwenzake wa Marekani John Kerry mjini Lausanne siku ya Jumamosi Oktoba 15. REUTERS/Darren Ornitz

Licha ya hali ya mvutano kati ya Marekani na Urusi mikutano miwili kuhusu Syria itafanyika mwishoni mwa wiki hii, na kuhudhuriwa na mawaziri wa Mambo ya nje Sergei Lavrov na John Kerry.

Matangazo ya kibiashara

Marekani ilisitiha rasmi mazungumzo na Urusi siku kumi zilizopita, na kusema kuwa uhalifu wa kivita ulitekelezwa katika mi wa Aleppo. Kwa upande wake, Moscow ilipinga kwa kura yake ya turufu azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu kusitishwaji wa mapigano katika mji wa Aleppo.

Lakini mbali na mvutano huo, wizara za mambo ya nje za nchi hizi mbili zinaendelea kufanya kazi kwa pamoja, kwani John Kerry na Sergei Lavrov wanatarajiwa kukutana mara mbili mwishoni mwa wiki hii.

Jumamosi, Oktoba 15, 2016, mkutano wa kwanza utafanyika katika mji wa Lausanne, nchini Uswisi, na Jumapili, mkutano wa pili utafanyika katika mji wa London, nchini Uingereza. Lengo la Marekani ni kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika mji wa Aleppo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani,John Kirby, anaonekana kuwa makini kuhusu mkutano huo. "Siahidi kwamba mikutano hii itafikia makubaliano mapya, mfumo mpya, mpango mpya. Lakini Waziri wa mambo ya Nje atashiriki katika mikutano hii ili kujaribu kupata mfumo ambao utapelekea kusitishwa kwa mapigano, kilicho muhimu zaidi, kuanza kupeleka misaada kwa walengwa. "

Urusi wala Marekani hawathibitisha kwamba Iran, mshirika wa Rais Bashar al-Assad, itashiriki katika mazungumzo haya yatakayofanyika mjini Lausanne.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, katika mahojiano kwenye televisheni ya Marekani, amezitaja Uturuki, Saudi Arabia na Qatar wanaounga mkono upinzani nchini Syria, kwamba kuna uwezekano wakashiriki katika mkutano huu wa kwanza.