KENYA-KENYA AIRWAYS

Hali ya sintofahamu katika shirika la ndege la Kenya Airways

Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways.
Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways. Wikipédia/Adrian Pingstone

Hali ya sintofahamu yaripotiwa kati ya usimamizi wa shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, na marubani. Kuanzia Jumatatu hii, shirika la marubani wa Kenya Airways (Kalpa), limetoa wito wa mgomo wa siku saba.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya mkutano na uongozi wa shirika hili Jumapili Oktoba 16, chama cha marubani wa Kenya Airways ameendelea kushikilia msimamo wake wa kuendesha mgomo. Marubani wanaomba kiongozi wa bodi ya shirika hilo, Dennis Awori, na mkurugenzi wake, Mbuvi Ngunze kujiuzulu. Wawili hao wanalaumiwa kutokuwa na uwezo wa kutafutia ufumbuzi wa matatizo yanayolikabili shirika la ndege la Kenya Airways.

"Hatuna imani katika mkakati wa uongozi wa Kenya Airways," Kapteni Paul Gichinga, katibu mkuu wa Kalpa, amesema.

Shirika la ndege la Kenya Airways lilishuhudia rekodi ya hasara ya Euro milioni 230 mwaka jana. Hali hii ilisababishwa na magaidi wa Al Shababkutokana na mashambulizi dhidi ya watalii nchini Kenya, kwa mujibu wa usimamizi wa shirika la ndege la Kenya Airways.

Marubani kwa upande wao, wanaona hali hiyo inatokana na uongozi mbovu. Mwaka 2011 hasa, shirika la ndege la Kenya Airways lilizindua mradi wake uliojulikana kwa jina la 'Mawingu', ambao ulikua mpango wa upanuzi ununuzi wa ndege mpya na ambapo lengo lilikuwa kuongeza safari za ndege ifikapo mwaka 2021. Lakini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na kuongezeka kwa vitendo vya ugaidi, mpango huu ulishindikana.

Tangu mwaka jana, Kenya Airways imechukua hatua kali ili kurekebisha usawa: kuwafuta kazi watu 600, sawa na 15% ya wafanyakazi wa shirika hilo, safari za ndege zimepunguzwa kutoka ndege 52 hadi 36. Kenya Airways inatarajia kupunguza hasara kutoka Euro milioni 100 hadi Euro milioni 43. Uongozi wa Kenya Airways unatambua upande mwingine kwamba kunahitajika Euro milioni 270 ya uwekezaji ili Kenya Airways iondokane na matatizo hayo.