MAREKANI-CLINTON-TRUMP

Clinton na Trump wachangia pamoja chakula mjini New York

Wagombea wawili katika kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani wakichangia chakula cha jioni kwenye meza moja wakati wa dhifa iliyoandaliwa mjini Astoria Walforf chini usimamizi wa Askofu Mkuu wa New York.
Wagombea wawili katika kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani wakichangia chakula cha jioni kwenye meza moja wakati wa dhifa iliyoandaliwa mjini Astoria Walforf chini usimamizi wa Askofu Mkuu wa New York. REUTERS/Jonathan Ernst

Hillary Clinton na Donald Trump walipata fursa ya kushirika katika dhifa Alhamisi usiku, huku wakirushiana vijembe kwa utani, kila mmoja akimkosoa mwenzake kwa sera zake. Hillary Clinton na Donald Trump walishiriki katika dhifa hiyo siku moja baada ya kushambuliana vikali kwenye mdahalo wa tatu na mwisho wa runinga.

Matangazo ya kibiashara

Bw Trump alizomewa alipofanya mzaha kwamba mpinzani huyo wake huwachukia Wakatoliki. Lakini alijaribu kuwaweka sawa waliohudhuria mdahalo huo, aliposema kuwa Michele Obama anapotoa hutuba anaonekana kuwa ni mtu mwenye maana, lakini inapofikia mkee wake Melania Trump kutoa hotuba kama hiyo anakosolewa.

"Usiku wa kuamkia leo, nilimwita Hillary mwanamke mbaya, lakini mambo haya yote yanategemea. Baada ya kumsikiliza Hillary akiongea na kuongea, sidhani Rosie O'Donnell ni mbaya tena, " amesema Bw Trump.

Kwa upande wake Hillary Clinton amesema mpinzani huyo wake wa chama cha Republican anaendesha "kampeni ya chuki na kuwagawanya watu" na kwamba hafai kuwa rais wa Marekani.

"Nimelazimika kumsikiliza Donald Trump kwa midahalo mitatu. Sasa nimeketi karibu na Donald Trump muda mrefu kuliko maafisa wake wa kampeni," amesema Hillary Clinton.

"Nimefurahia sana kusikia Donald alidhani nilitumia dawa za kuchangamsha mwili (kabla ya mdahalo). Ni kweli nilitumia. Kunaitwa kujiandaa," ameongeza Bii Clinton.

Kama desturi kwa wagombea wanaowania kinyang'anyiro cha urais nchini Marekani kuanzia kwa Nixon na Kennedy waliwahi kushiriki katika dhifa ya kudumisha upendo iliyoandaliwa katika mji wa Walforf Astoria chini ya usimamizi wa Askofu Mkuu wa New York. Mila hii inataka wagombea wote wawili wakosoane kati yao kwa utani, na hali hii hupelekea kukuza upendo na udugu.

Dhifa hiyo ya Wakfu wa Ukumbusho wa Alfred E Smith mjini New York hufanyika kila baada ya miaka minne na kuwashirikisha wagombea urais.