AFRIKA KUSINI-ZUMA

Ripoti kuhusu uhalifu wa rushwa katika viwango vya juu serikalini yatolewa

Tuhuma za rushwa zamkabili rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Tuhuma za rushwa zamkabili rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma. REUTERS/Siphiwe Sibeko

Ripoti rasmi, ambayo ni ya aibu kwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma inayomuhusisha katika uhalifu wa rushwa, imechapishwa JUmatano hii jioni nchini Afrika Kusini kufuatia uamuzi wa mahakama. Ripoti hii imeitaka Ofisi ya mashitaka na polisi kuchunguza uwezekano wa "uhalifu" wa rushwa uliotekelezwa na vigogo serikali.

Matangazo ya kibiashara

Ripoti hii inabaini kuwa imetambua ushahidi unaoonyesha kuwa uhalifu huenda umefanyika katika viwango vya juu serikalini.

Ripoti hii ni pigo kwa Zuma baada ya kuhusishwa kwenye tuhuma za rushwa.

Awali Mahakama kuu nchini Afrika Kusini, imemuagiza mkurugenzi wa ofisi ya mkaguzi wa mali ya uma, kuchapisha ripoti ya tuhuma za rushwa dhidi ya Rais Jacob Zuma.

Ripoti hiyo inasema kuwa imetambua ushahidi unaoonyesha kuwa uhalifu huenda umefanyika katika viwango vya juu serikalini.

Uamuzi wa mahakama umekuja, baada ya Jumatano asubuhi, mawakili wa Rais Zuma kuiambia mahakama kuwa, mteja wao ameamua kuondoa pingamizi lililokuwepo mahakamani kuzuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

Uamuzi wa mahakama umekuja, wakati huu maelfu ya waandamanaji wakiwa wamekusanyika kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Pretoria kushinikiza Rais Zuma kuondoka madarakani.

Ripoti ya mkaguzi wa mali ya uma inahusu uchunguzi uliofanywa kuhusu uhusiano alio nao Rais Zuma na familia ya kihindi ya Gupta, ambapo anadaiwa kuwa familia hiyo imekuwa ikimchagulia baadhi ya mawaziri.

Idara ya kupambana na rushwa nchini Afrika Kusini imependekeza kuwa tume ya uchunguzi inayosimamiwa na hakimu ibuniwe ndani ya siku 30, kuchunguza madai ya ushawishi wa familia ya Gupta kwa uteuzi wa nyadhifa za serikali.

Tume hiyo mpya itawasilisha matokeo yake kwa rais ndani ya siku 180.

Akisoma uamuzi wa mahakama, jaji kiongozi kwenye kesi hiyo, Dustan Mlambo, amesema "Mkaguzi mkuu wa mali za uma anaagizwa kuitoa ripoti hiyo sio zaidi ya saa kumi na moja jioni."

Aliyekuwa mkaguzi mkuu wa mali za uma, Thuli Mandonsela, alimaliza kuandika ripoti yake mwezi mmoja uliopita kuhusu uhusiano wa familia ya Gupta na Rais Zuma, siku chache tu kabla ya muda wake kuhudumu ofisini kutamatika.

Ripoti hii ilikuwa ichapishwe October 14 lakini Rais Zuma alienda mahakama kuzuia kuchapishwa kwa ripoti hiyo.

Makundi mbalimbali ya upinzani nchini Afrika kusini yamekuwa yakifanya maandamano kwenye miji mkubwa nchini Afrika kusini kupinga uongozi wa rais Jacob Zuma.