DRC-SIASA

Upatanishi wa makanisa kutoka Afrika waondoa DRC bila kukutana na Kabila

Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015.
Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015. © AFP PHOTO / CARL DE SOUZA

Ujumbe wa Shirikisho la Makanisa kutoka Afrika (AACC) uliwasili tangu mwanzoni mwa wiki iliyopita nchini DRC. Ujumbe huu, ukiongozwa na Askofu Valentine Mokiwa, mwenyekiti wa shirikisho hilo, ulikuja kuhubiri amani. Lakini unaondoka mjini Kinshasa Jumatatu hii, Novemba 7 bila kukutana na rais Joseph Kabila na kambi ya wanasiasa wanaomuunga mkono.

Matangazo ya kibiashara

Ni ujumbe wa upatanishi na ulikua unataka kujaribu kuelewa kinachosababisha mgogoro wa sasa kuendelea kushuhudiwa nchini humo. Ujumbe huu unaoongozwa na Askofu Valentine Mokiwa kutoka Tanzania uliwasili katika mji wa Kinshasa mwanzoni mwa juma lililopita ukiwa na lengo la kuwasihi wanasiasa wote kuketi kweny meza ya mazungumzo kwa lengo la kudumisha amani na maendeleo ya nchi yao.

Ujumbe huu ulikutana kwa mazungumzo na Askofu Marini Bodho, rais wa heshima wa Seneti, Mwakilishi wa Papa nchini DRC, wakuu wa madhehebu ya dini, mabalozi wa Marekani, wa Umoja wa Ulaya na wa nchi za Afrika. Pia ujumbe huu ulikutana na mkuu wa Monusco, Naibu Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchauguzi (CENI) na kiongozi wa chama cha UDPS pia Mwenyekiti wa Kamati ya Wazee wa busara wa muungano wa upinzani wa Rassemblement Etienne Tshisekedi.

Askofu Valentine Mokiwa na wanachama wa ujumbe wake walijadili masuala yanayohusiana na hali ya nchi hiyo. Waligusia hasa mgogoro wa kisiasa na matukio ya tarehe 19 na 20 Septemba, huku wakielezea masikitiko yao kuhusu vifo vya watu wengi waliouawa wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na upinzani. "Hali hii istokei tena", wamependekeza wanachama wa AACC, ambao wanaondoka mjini Kinshasa Jumatatu hii bila kukutana na Rais Joseph Kabila na wawakilishi wa vyama vinavyomuunga mkono.