MAREKANI-SIASA-UCHAGUZI

Wananchi wa Marekani kumchagua rais wao Jumanne hii

Donald Trump na Hillary Clinton wagombea katika uchaguzi wa urais Marekani, Novemba 8, 2016.
Donald Trump na Hillary Clinton wagombea katika uchaguzi wa urais Marekani, Novemba 8, 2016. REUTERS/Shannon Stapleton

Wananchi wa Marekani watapiga kura leo Jumanne kumchagua rais wao, ambaye atamrithi Rais Barack Obama. Wagombea katika uchaguzi huo ni Donald Trump wa chama cha Republicana na Hillary Clinton wa chama cha Democratic. 

Matangazo ya kibiashara

Uchaguzi huu umekua na ushindani mkubwa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mpaka siku ya leo ya uchaguzi watu wameendelea kutoa tathmini zao kuhusu nani ataibuka mshindi.

Awali wagombea hawa wawili walionekana katika mijadala kwenye runinga wakitupia vijembe na kila mmoja kumshutumu mwengine kwa makosa aliyofanya kwamba hana hadhi ya kuliongoza taifa la Marekani.

Hata hivyo uamuzi wa mwisho wa mshindi wa urais nchini Marekani huamuliwa na wajumbe 538 wanaoteuliwa kutoka katika majimbo yote 50 nchini humo.

Hatua hii huja mara baada ya raia wa kawaida kupiga kura katika vituo mbalimbali na kumchagua rais wao wanaotaka awaongoze kwa muda wa miaka minne.

Mgombea anastahili kupata angalau kura 270 za wajumbe kati ya 538 ili kuwa rais wa Marekani na wajumbe hao huamua mshindi kwa namna watu walivyopiga kura katika majimbo mbalimbali.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2012, Barrack Obama alipata ushindi baada ya kuchaguliwa kwa kupata kura 65,915,795 huku mpinzani wake Mitt Romney akipata kura 60,933,504.

Wajumbe walipopiga kura, Obama alipata ushindi wa wajumbe 332 dhidi ya Romney aliyepata kura ya wajumbe 206 katika uchaguzi huo.

Kuelekea Uchaguzi huu, kuna majimbo ambayo ni ngome ya chama cha Republican sawa na Democratic lakini kuna majimbo mengine kama Florida, Pennsylvania na Ohio ambayo hayana msimamo wa pande zot, hayo ndio majimbo ambayo yataamua mshindi wa uchaguzi huu.

Pamoja na kumchagua rais siku ya Jumanne, raia wa Marekani watapiga kura kuwachagua wawakilishi 435 wanaohudumu kwa miaka miwili.