MAREKANI-UCHAGUZI 2016

Matokeo ya uchaguzi katika majimbo mbalimbali

Wananchi wa Marekani walipiga kura Jumanne wiki hii kumchagua rais wao, ambaye atamrithi Rais Barack Obama anayemaliza muda wake. Uchaguzi huu umekua na ushindani mkubwa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi, wiki kadhaa zilizopita.

Ramani ya Marekani.
Ramani ya Marekani. AP
Matangazo ya kibiashara

Wagombea wakuu katika uchaguzi huo ni Donald Trump wa chama cha Republican na Hillary Clinton wa chama cha Democratic.

Bi.Clinton wa chama cha Democratic ikiwa atachaguliwa ataweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kuwa rais wa taifa hilo lenye nguvu duniani.

Donald Trump naye anayewania wadhifa huo kwa  chama cha Republican akifanikiwa kupata ushindi, atakuwa rais wa kwanza mfanyibiashara asiye na uzoefu wa kisiasa kuongoza taifa hilo.

Uchaguzi huu unaangaziwa kwa makini sana duniani hasa baada ya kampeni yenye nguvu kati ya wagombea hao kumalizika siku  ya Jumatatu, huku wagombea hao wawili wakiwarai wapiga kura kuwachagua.

Wakazi wa majimbo ya Mashariki yanayopakana na Bahari ya Atlantic ndio waliokuwa wa kwanza kuanza kupiga kura na katika vituo mbalimbali, foleni ndefu za wapiga kura zilishuhudiwa.

Awali wagombea hawa wawili walionekana katika mijadala kwenye runinga wakitupia vijembe na kila mmoja kumshutumu mwengine kwa makosa aliyofanya kwamba hana hadhi ya kuliongoza taifa la Marekani.

Hata hivyo uamuzi wa mwisho wa mshindi wa urais nchini Marekani huamuliwa na wajumbe 538 wanaoteuliwa kutoka katika majimbo yote 50 nchini humo.

Hatua hii huja mara baada ya raia wa kawaida kupiga kura katika vituo mbalimbali na kumchagua rais wao wanaotaka awaongoze kwa muda wa miaka minne.

Mgombea anastahili kupata angalau kura 270 za wajumbe kati ya 538 ili kuwa rais wa Marekani na wajumbe hao huamua mshindi kwa namna watu walivyopiga kura katika majimbo mbalimbali.

Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2012, Barack Obama alipata ushindi baada ya kuchaguliwa kwa kupata kura 65,915,795 huku mpinzani wake Mitt Romney akipata kura 60,933,504.

Wajumbe walipopiga kura, Obama alipata ushindi wa wajumbe 332 dhidi ya Romney aliyepata kura ya wajumbe 206 katika uchaguzi huo.

Hata hivyo kuna majimbo ambayo ni ngome ya chama cha Republican sawa na Democratic lakini kuna majimbo mengine kama Florida, Pennsylvania na Ohio ambayo hayana msimamo wa pande zote, hayo ndio majimbo ambayo yataamua mshindi wa uchaguzi huu.

Pamoja na kumchagua rais siku ya Jumanne, raia wa Marekani wamepiga kura kuwachagua wawakilishi 435 wanaohudumu kwa miaka miwili.