MAREKANI-TRUMP-SIASA

Maelfu ya raia wamiminika mitaani dhidi ya ushindi wa Trump

Rais Donald Trump amesema kipaumbele chake kitakuwa kufufua na kuimarisha miundo mbinu ya nchi hiyo pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa hilo maradufu.
Rais Donald Trump amesema kipaumbele chake kitakuwa kufufua na kuimarisha miundo mbinu ya nchi hiyo pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa hilo maradufu. REUTERS/Mike Segar

Maelfu ya raia nchini wamemiminika mitaani katika miji mbalimbali na majimbo kadhaa nchini Marekani wakipinga ushindi wa Donald Trump. Hata hivyo Rais anayemaliza muda wake Barack Obama amemwalika Rais mteule wa Marekani Donald Trump katika White House.

Matangazo ya kibiashara

Mamia kwa maelfu ya waandamanaji wanaompinga Donald Trump walikusanyika nje ya jumba kuu la Bw Trump, Trump Tower eneo la Manhattan jijini New York Jumatano jioni, wakibeba mabango yaliyokuwa na ujumbe "Not my president" ikimaanisha 'Si Rais wangu', pamoja na mabango mengine.

Awali polisi waliweka vizuizi vya saruji pamoja na kuchukua hatua nyingine za kiusalama nje ya jumba hilo ndefu linalopatikana barabara ya 5th Avenue, jumba ambalo huenda likawa makao makuu ya Bw Trump wakati wa kipindi cha mpito kabla ya kuingia White House.

Kuliripotiwa pia taarifa za waandamanaji kuziba lango la kuingia jumba la Trump Tower mjini Chicago Jumatano jioni, wakiimba: "No Trump, No KKK, No Fascists USA, No my president" ikimaanisha 'Hatumtaki Trump, Hatutaki KKK, Hatutaki Wafashi Marekani, Si rais wangu'.

Mjini Oakland, California, na Portland, Oregon, waandamanaji waliteketeza bendera za Marekani.

Obama amwalika Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amemwalika Rais mteule wa Marekani Donald Trump katika White House.

Rais Obama amesema katika mkutano wao watajadili kuhusu shughuli ya mpito na kupokezana madaraka.

Amesma anataka shughuli hiyo iwe ya haraka na bila matatizo.

Msemaji wa White House Josh Earnest amesisitiza kwamba Bw Obama atakuwa na uwazi kuhusu kuhakikisha shughuli laini ya mpito atakapokutana na Bw Trump, ingawa aliongeza kwamba: "Sijasema kwamba utakuwa mkutano rahisi."

Rais huyo mteule atasindikizwa kwenda White House Alhamisi na mkewe, Melania, ambaye atakutana na Mke wa Obama, Michelle.

Bw Obama, aliyempongeza mrithi huyo wake kwa njia ya simu mapema Jumatano, alisema si siri kwamba yeye na Bw Trump wana tofauti nyingi.

Lakini aliongeza kwamba wanataka kuhakikisha wanalinda maslahi ya taifa na kwamba alitiwa moyo na yale Bw Trump alikuwa amesema usiku uliotangulia.

Kundi la kushughulikia shughuli ya mpito la Bw Trump litaongozwa na Chris Christie, gavana wa New Jersey, na lina wiki 10 kukamilisha maandalizi hayo.

Donald Trump, rais wa 45

Donald Trump kutoka chama cha Republican atakuwa rais wa 45 wa Marekani baada ya kupata ushindi wa kushangaza dhidi ya Hillary Clinton wa chama cha Democratic, chake Rais Obama.

Bw Obama alifanya kampeni kali kumzuia Bw Trump kushinda, na alisema hafai kuongoza.

Rais Obama amehimiza umoja na Bi Clinton amewaambia wafuasi wake kwamba Bw Trump anafaa kupewa "nafasi ya kuongoza".

Bw. Obama amewahimiza Wamarekani wote kukubali matokeo ya uchaguzi wa Jumanne.
"Tunatafuta ufanisi wake katika kuunganisha na kuongoza nchi hii," Rais Barack Obama alisema kuhusu Trump.

Ahadi za Trump ndani ya siku 100 za kwanza madarakani

Wakati wa hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi mapema Jumatano, Bw Trump aliahidi kuponya vidonda vya migawanyiko, baada ya uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali, na kuahidi kwamba atakuwa "rais wa Wamarekani wote".

Rais huyo mteule, ambaye hajawahi kuhudumu katika wadhifa wowote wa kuchaguliwa au kuteuliwa serikalini, amesema kipaumbele chake kitakuwa kufufua na kuimarisha miundo mbinu ya nchi hiyo pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa hilo maradufu.

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha Republican Reince Priebus alisema: "Donald Trump anachukulia hili kwa uzito sana," na kuongeza kwamba mfanya biashara huyo tajiri atatumia uwezo wake wa kutetea na kufanikisha mikataba ya kibiashara kuhakikisha mambo mema "yanatendeka kwa Wamarekani" haraka iwezekanavyo.