Alain Juppé kupambana na François Fillon katika mjadala wa kura za mchujo

François Fillon na Alain Juppé waliopata ushindi katika duru ya kwanza ya kura za mchujo watapambana Alhamisi hii usiku katika mjadala wa mwisho kwenye televisheni. Wawili hao watakua pamoja, wakisimama nyuma ya kio huku wakitazamwa na watu 60 ambao watakua wamealikwa kuhudhurika mjadala huo.

Alain Juppé na François Fillon wakati wa mjadala wa pili kwa kura za mchujo, Novemba 3, 2016.
Alain Juppé na François Fillon wakati wa mjadala wa pili kwa kura za mchujo, Novemba 3, 2016. REUTERS/Eric Feferberg
Matangazo ya kibiashara

François Fillon na Alain Juppé watahojiwa na waandishi wa habari watatu na kila atapewa dakika 2 ili kujibu swali. Katika ingwe ya pili Alain Juppe na François Fillon watajadili pamoja mada tatu: majukumu ya kila mmoja atakapobahatika kuchaguliwa kuwa rais? Nini jamii ipi unayoitaka ? Na upi mtazamo wako kwa Ufaransa? Mjadala huu wa nne na wa mwisho, ambao utadumu saa 1:40, utaanza saa 2:00 usiku saa za kimataifa (sawa na saa 5:00 usiku saa za Afrika ya mashariki).

Alain Juppé atuhumiwa kukigawa chama cha mrengo wa kulia

Katika makala iliyochapishwa Alhamisi hii, Novemba 24 katika gazeti la Le Figaro, wabunge wengi wa chama cha mrengo wa kulia wametoa wito kwa utulivu baada ya Alain Juppé kumshambulia kwa maeneno makali François Fillon.

Alain Juppé, Meya wa mji wa Bordeaux ambaye alishindwa kwa alama 15 dhidi ya mshindani wake François Fillon katika duru ya kwanza ya kura za mchujo Jumapili iliyopita, alikashifu msimamo wa mshindani wake kuhusu utoaji mimba, na kufuta baadhi ya idara katika sekta ya uuma. Wengi wamemtuhumu kwamba ana lengo la kusambaratisha chama cha mrngo wa kulia.

Katika makala haya ya Le Figaro, Wabunge na Maseneta 215 wamesikika wakisema "pamoja, tujadili hali hii." Wawakilishi hawa wanalaani 'kashfa' za Alain Juppe dhidi ya François Fillon, wakati ambapo tangu kutangazwa kwa matokeo ya duru ya kwanza ya kura za mchujo, Meya wa mji wa Bordeaux hakusita kumuaibisha mpinzani wake katika kura za msingi. Wawakilishi hao kutoka chama cha mrengo wa kulia wametoa wito wa kuheshimiana katika mjadala.

Jumatano wiki hii wabunge wengi wa Bunge la Ufaransa walitoa wito wa kumkanya Alain Juppé.

Kwa mujibu wa utafiti wa Ifop kwa niaba ya gazeti la Paris Match, iTELE na Sud Radio, François Fillon atashinda kwa 65% ya kura katika duru ya pili ya kura za mchujo Jumapili ijayo, dhidi ya 35% ya kura atakazopata Alain Juppé.