MAREKANI-SIASA-TRUMP

Donald Trump: Sintokubali kura kuhesabiwa upya

Donal Trump aliibuka mshindi kwa kupata kura za wajumbe wa majimbo lakini Clinton akashinda kura za wananchi.
Donal Trump aliibuka mshindi kwa kupata kura za wajumbe wa majimbo lakini Clinton akashinda kura za wananchi. REUTERS/Carlo Allegri

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amedai kuwa alishinda kura za wapiga kura nchini humo licha ya matokeo kuonesha kuwa mshindi alikuwa ni Hillary Clinton.

Matangazo ya kibiashara

Trump amedai kuwa Clinton ameshinda kura za wananchi kwa sababu wapiga kura wasio halali walipiga kura mapema mwezi huu.

Matamshi haya yamekuja baada ya Bi.Clinton kusema anaunga mkono kuhesabiwa upya kwa kura hasa katika jimbo la Wisconsin.

Trump aliibuka mshindi kwa kupata kura za wajumbe wa majimbo lakini Clinton akashinda kura za wananchi.

Kampeni ya Hillary Clinton, hivi karibuni ilidai kuwa itaungana na jitihada za kutaka kuhesabiwa kwa kura katika baadhi ya maeneo nchini Marekani, zilizoanzishwa na mgombea wa Green Party, Jill Stein, aliyekusanya mamilioni ya dola ili kura katika jimbo la Wisconsin zihesabiwe upya.

Hata hivyo mshauri wa kampeni hiyo, Marc Elias, alidai kuwa uchunguzi wao wenyewe haujaweza kubaini ushahidi wowote wa udukuzi katika mifumo ya kupiga kura.

Bw Elias alidai kuwa licha ya kampeni yake kutopinga matokeo, imeamua kushiriki katika jitihada za kuhakikisha kuwa matokeo hayo yako sawa kwa pande zote. Hata hivyo Rais mteule, Donald amepinga kurudiwa kwa uhesabuji kura na kusema kuwa uchaguzi umemalizika.

Bw Trump pia amekikosoa Green Party na kudai kuwa jitihada zake ni za ulaghai huku akimshutumu mgombea wake, Jill Stein kwa kutaka kujikusanyia fedha ambazo hatozitumia kwa shughuli hiyo.