Bloomberg: Kabila na familia yake wajitajirisha kupitia mali ya DRC

Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015.
Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015. © AFP PHOTO / CARL DE SOUZA

Katika utafiti uliyoendeshwa Alhamisi hii na shirika la habari la Marekani linalojihusisha katika masuala ya kiuchumi linasema kuwa "Kabila na familia yake wameunda pamoja mtandao wa kibiashara ambao unazishikila sekta zote za uchumi wa Congo na tayari mtandao huo umezipatishia familia zao mamilioni ya Dola. "

Matangazo ya kibiashara

"Tangu mwaka 2003, familia ya Kabila ilianzisha mtandao wa kimataifa wa kibiashara na kushirikishwa katika makampuni yasiyopungua 70," limeandika shirika la habari la Bloomberg, huku likiongeza kuwa Kabila, mkewe, watoto wake wawili na ndugu zake wanane wanadhibiti zaidi ya vibali 120 vya uchimbaji wa dhahabu, almasi, shaba, cobalt na madini mengine "nchini DRC.

Mtandao wa kimataifa wa biashara

Licha ya madini, familia inajihusisha pia katika sekta ya "benki, kilimo, usambazaji mafuta, usafiri wa anga, ujenzi wa barabara, hoteli, uuzaji wa dawa, mashirika ya usafiri, biashara na klabu za usiku, "wameongeza waandishi wa waliofanya uchunguzi huo, huku wakiyataja makampuni yaliyoko Congo, lakini pia nchini Marekani, Panama, Tanzania na katika kisiwa cha Niue.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg, kiasi cha maslahi haya ya kiuchumi "kinaweza kusaidia kuelewa sababu ambayo rais Joseph Kabila anapuuzia wito wa Marekani, wa Umoja wa Ulaya na idadi kubwa ya raia wa Congo wa kuachia ngazi wiki ijayo."

Shirika la habari la Bloomberg linasema ripoti yake ni matokeo ya kazi ya mwaka mmoja iliyofanywa na waandishi wa habari watatu kuhusu "mtandao wa biashara" wa familia ya rais Joseph Kabila huku likiwa na vielelezo kadhaa vya mahojiano na "maelfu ya nyaraka ya makampuni na nyaraka za mahakama."

Nchi tajiri, raia masikini

Nchi ya DRC inajulikana kwa utajiri wake wa maliasili na umaskini uliokithiri wa raia wake karibu 90% ya raia wa DRC wanatumia chini ya Dola 1.25 kwa siku, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Joseph Kabila aliingia madarakani baada ya kuuawa kwa baba yake Laurent-Desire Kabila, muasi ambaye alichukua madaraka na kuwa rais kwa mtutu wa bunduki na kufaulu kumtimua dikteta Mobutu Sese Seko mwezi Mei 1997.

Joseph Kabilila alichaguliwa kuwa rais mwaka 2006 na kuchaguliwa kwa mara nyingine tena mwaka 2011 katika uchaguzi uliogubikwa na udanganyifu mkubwa.

Muhula wa pili wa rais Joseph Kabila unamalizika tarehe 20 Desemba na katiba haimruhusu kuwania kwa muhula wa tatu.