Joseph Kabila aendelea kupata shinikizo la kujiuzulu
Imechapishwa:
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila anaendelea kupokea shinikizo jamii ya kimataifa kutokana na hali inayoendelea nchini mwake na uamuzi wake wa kukataa kung'atuka madarakani baada ya kumaliza mihula miwili kama inavyosema Katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hata hivyo Ufaransa imesema iko tayari ikutuma ombi kwa umoja wa ulaya la kumwekea vikwazo rais Joseph Kabila iwapo ataendelea kushikilia maamlaka.
Hayo yakijiri Ujerumani imehairisha majadiliano ya kuipa DR Congo msaada wa miradi ya maendeleo.
Itakumbukwa kwamba muhula wa Kabila ulimalizika siku ya Jumanne Desemba 20.
Wakati huo huo Maskofu wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaoongoza mazungumzo ya kisiasa kati ya wanasiasa wa upinzani na wale wa serikali, wamesema wanataka mwafaka upatikane kabla ya Sikukuu ya Krismasi siku ya Jumapili.
Mazungumzo yalitarajiwa kurejelewa leo lakini hilo halijawezekana kutokana na maandamano yalishuhidiwa hasa jijini Kinshasa na Lubumbashi na kusabisha vifo vya watu 19 na wengine 45 kujeruhiwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa.
Bado hali ni ya wasiwasi lakini sio kama jana kama anavyoleza Reubens Mikindo, Naibu Katibu Mkuu chama cha UDPS cha Etienne Tshisekedi akiwa jijini Kinshasa.