GAMBIA-SIASA

Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Gambia yaahirishwa

Rais wa Gambia Yaya Jammeh, apinga kuondoka mamlakani.
Rais wa Gambia Yaya Jammeh, apinga kuondoka mamlakani. ISSOUF SANOGO / AFP

Mahakama kuu nchini Gambia imeahirisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini humo iliyowasilishwa na Rais Yahya Jammeh hadi Januari 10 mwaka Ujao.

Matangazo ya kibiashara

Jammeh ametaka kwamba matokeo ya uchaguzi huo uliompa ushindi Adama Barrow yabatilishwe. Mahakama hiyo ambayo mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu Emmanuel Fagbenle imeamuru kuwa, kesi hiyo iahirishwe kwa sababu Tume Huru ya Uchaguzi ya Gambia ilikuwa bado haijapokea nyaraka za kesi.

Katikati mwa juma hili Rais wa Gambia Yahya Jammeh alisisitiza kuwa hataondoka madarakani muhula wake utakapomalizika tarehe 19 mwezi Januari mwaka ujao.

Jammeh ambaye alikuwa akisema kuwa mpinzani wake Adama Barrow aliyetangazwa mshindi hakushinda kwa haki, amesisistiza kuwa hatatishwa na yeyote.

Juhudi za viongozi wa nchi za Afrika Magharibi kumshawishi rais Jammeh kuondoka madarakani hazijafua dafu.

Juma lililopita upinzani nchini Gambia ulionya kuwa endapo rais anayemaliza muda wake nchini humo Yahya Jammeh atakataa kuondoka Madarakani atachukuliwa kama muasi. Yahya Jammeh alirejelea kauli yake hivi karibuni baada ya kutambua ushindi wa mshindani wake Adama barrow, na kutaka kura zirudi kuhesabiwa upya.

Hivi karibuni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi, Mohamed Ibn Chambas, alisema kuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh anapaswa "kuwa tayari kukabidhi madaraka" ifikapo mwezi Januari mwakani.

Bw ibn Chambas alisema Umoja wa Mataifa hautaendelea kufumbia macho viongozi ambao hushindwa na kisha baadaye wanatumia nguvu kwa kuchukua madaraka.

"Upinzani ulishinda uchaguzi, ambao uliku halali, " amesema Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa wa Ban Ki-moon katika Afrika ya Magharibi.

Jumanne Desemba 13 Marais wanne kutoka Afrika Magharibi walifanya ziara katika mji mkuu wa Gambia, Banjul na kujaribu kumshawishi Yahya Jammeh kukubali kushindwa katika uchaguzi wa urais na kukabidhi madaraka, bila mafanikio.

Mihula ya miaka mitano ya Bw Jammeh itamalizika Januari 19, Mohamed Ibn Chambas amesema, huku akiongeza kuwa "atakuwa tayari kukabidhi madaraka" tarehe hiyo.