ISRAEL-NETANYAHU-RUSHWA

Waziri mkuu wa Israel ahojiwa kwa tuhuma za rushwa

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mke wake Sara , Desemba 4, 2014.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mke wake Sara , Desemba 4, 2014. REUTERS/Nir Elias/Files

Polisi nchini Israel wamemhoji Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, kuhusu madai ya kupokea zawadi kutoka kwa wafuasi na wafanyabiashara mbalimbali kinyume na sheria.

Matangazo ya kibiashara

Netanyahu alihojiwa kwa muda wa saa tatu katika makazi yake mjini Jerusalembaada ya kutuhumiwa kupokea "zawadi haramu," alisema msemaji wa polisi katika taarifa yake.

"Hakuna maelezo zaidi yanayoweza kutolewa kwa wakati huu," ilisema taarifa hiyo.

Wizara ya Sheria pia imethibitisha katika taarifa yake kuwa Netanyahu alihojiwa na kitengo cha polisi ya kupambana dhidi ya rushwa cha "Lahav 443".

Lengo la mahojiano haya ni kubaini ikiwa Netanyahu, alipokea zawadi hizo kinyume na sheria kutoka kwa matajiri wanaomuunga mkono.

Uchunguzi huu pia unalenga kubaini ikiwa Netanyahu alipokea Maelfu ya fedha kutoka kwa wafanyibiashara kutoka nje ya nchi lakini, pia Waisraeli wanaomuunga mkono.

Benjamin Netanyahu alihojiwa kwa amri ya mwanasheria mkuu wa Israel.

Hata hivyo Benjamin Netanyahu alikana kuhusika katika jambo hilo, huku akisema malalamiko yanayotolewa dhidi yake kuwa alikua akipokea zawadi kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali ni uzushi mtupu na kusema kuwa maadui wake wa kisiasa wanatumia mbinu hiyo kuiangusha serikali yake.

Licha ya tuhuma hizi, Netanyahu amekiri kuwa mwaka 2001, alipokea Dola za Marekani 40,000 kutoka kwa tajiri kutoka Ufaransa Arnaud Mimran, wakati hakuwa Ofisini, fedha alizotumia kuinua sifa ya Israel nje ya nchi.

Netanyahu na mke wake Sara wamehusishwa katika kashfa mbalimbali kipindi cha nyuma, ikiwemo tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za serikali.