SOMALIA-SIASA

Somalia yampata Spika mpya wa Bunge

Mohammed Osman Jawari amechaguliwa tena Spika wa Bunge nchini Somalia, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi wa urais. Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press (AP) Mohammed Osman Jawari amechaguliwa tena Spika wa Bunge la Somalia.

Wabunge wa Somalia wakila kiapo wakati Desemba 27, 2016.
Wabunge wa Somalia wakila kiapo wakati Desemba 27, 2016. REUTERS/Feisal Omar
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu mfumo wa uongozi wa ukoo unaoendesha siasa za Somalia, kuchaguliwa kwa Bw. Jawari ambaye ni kutoka ukoo wa Digil na Mirifle, kuna maanisha Sharif Hassan Sheikh Adan, ambaye ni rais wa jimbo la Kusini Magharibi atalazimika kujiondoa katika mbio hizo za urais kwa sababu anatoka ukoo mmoja na Spika.

Wabunge ndio wanamchagua rais tofauti na mfumo wa kawaida ambapo wananchi wanashiriki zoezi hilo moja kwa moja.

Jumla ya wabunge 259 walishiriki zoezi hilo licha ya ulinzi mkali katika jumba la mafunzo ya polisi.

Uchaguzi wa urais nchini Somalia umeahirishwa mara kadhaa kufuatia madai ya udanganyifu na matumizi ya vitisho.

Tarehe rasmi ya uchaguzi haijatolewa lakini maafisa wanasema huenda ikawa baadaye mwezi huu wa Januari.

Wagombea wakuu waliosalia ni kutoka koo mbili kubwa za Hawiye na Darod.

Somalia iko katika harakati ya kujiimarisha upya baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu miongo kadhaa.

Machafuko na migogoro kwa misingi ya ukoo na vitisho vya kundi la Al shabab linalofutilia mbali demokrasia ya nchi za magharibi ni baadhi ya mambo yanayokwamisha kufikia hatua hiyo.