Yahya Jammeh: Siondoki madarakani
Rais wa Gambia Yahya Jammeh ametangaza kwamba hatoondoka mamlakani kabla ya mahakama kutoa uamuzi kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Desemba mwaka jana.
Imechapishwa:
Tangazo hilo linakuja siku moja baada ya mahakama ya juu kutangaza Jumanne wiki hii kwamba imeahirisha kusikiliza kesi ya uchaguzi mkuu hadi mwezi Mei.
Katika hotuba yake katika runinga ya taifa, rais Yahya Jammeh pia amesisitiza matamshi yake ya hapo awali ya kushtumu mataifa ya kigeni kwa kuingilia siasa za nchi yake.
Hata hivyo Rais mteule Adama Barrow amesema kuwa ataapishwa wiki ijayo.
Rais Yahya Jammeh awali alikubali kushindwa katika uchaguzi huo, lakini siku chache baadaye alikataa kuwa hakishindwa na badala yake aliwasilisha kesi mahakamani akibaini kwamba Tume ya Uchaguzi ilibadilisha baadhi ya matokeo.
Lakini Tume ya Uchaguzi inasisitiza kuwa matokeo ya uchaguzi hayakuathiriwa na kwamba mfanyibiashara Adama Barrow alishinda kwa kura chache.
Wapatanishi kutoka eneo hilo wakiongozwa na Nigeria wanatarajiwa nchini Gambia siku ya Ijumaa ili kumshinikiza kukubali kushindwa kufuatia uchaguzi huo wa mwezi Disemba