MALI-UFARANSA-AFRIKA-UCHUMI

Suala la uchumi kujadiliwa katika mkutano kati ya Afrika na Ufaransa mjini Bamako

Sehemu ambapo mkutano kati ya viongozi wa Afrika na Ufaransa utafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14Januari, 2017 mjini Bamako, nchini Mali.
Sehemu ambapo mkutano kati ya viongozi wa Afrika na Ufaransa utafanyika kuanzia tarehe 13 hadi 14Januari, 2017 mjini Bamako, nchini Mali. RFI/Paulina Zidi

Viongozi wanaoshiriki mkutano wa kilele kati ya Afrika na Ufaransa mjini Bamako, nchini Mali watajadili Ijumaa hii Januari 13 suala la uchumi. Alhamisi usiku viongozi sitini wa makampuni ya Ufaransa, wakiongozwa na Medef, chama cha waajiri nchini Ufaransa, waliwasili katika mji mkuu wa Mali.

Matangazo ya kibiashara

Wajumbe wa waajiri kutoka nchi kadhaa za Afrika pia watashiriki mkutano huo, ikiwa ni fursa kwa sekta ya binafsi nchini Ufaransa kutafuta ushirikiano na makampuni mbalimbali barani Afrika. Katika kipindi cha miaka 10, makampuni ya Hexagone yalipoteza karibu nusu ya wateja katika Ukanda wa kusini mwa Sahara.

Zaidi ya viongozi 40 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo wa 27 wa utakaojadili mambo ya Usalama na Jamii.

Vikosi vya usalama vimetawanywa mjini Bamako kwa muda wote wa mkutano, kwa hiyo kila mmoja atajihisi salama akiwa mjini Bamako, angalau basi kwa hizo siku mbili ambazo viongozi watakuwa mjini.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ataongoza viongozi hao kutoka nchi mbalimbali katika mji mkuu wa Mali, Bamako kwa ajili ya mkutano huo.

Kwa mujibu wa tume ya maandalizi, rais Abdoullah Coulibaly amesema Bamako ina uwezo wa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na itaugharamia.

Bajeti maalumu kwa ajili ya miundombinu ya mjini Bamako kuelekea maandalizi ya mkutano kumeleta sura mpya ya mji, kama vile ujenzi uliofanyika pembezoni mwa barabara.

Balozi wa Ufaransa Frédéric Clavier anasema, mkutano huu ndio utakuwa kithibitisho kwamba Mali hivi sasa iko tayari kuhodhi mikutano mikubwa ya kimataifa tena.

Mkutano huu unafanyika wakati ambapo kuna hali ya wasiwasi nchini humo kufuatia kuwepo kwa makundi mbalimbali ya wapiganaji.