Wabunge wa Somalia kumchagua Rais
Wabunge na Maseneta wa Somalia wanamchagua Jumatano hii rais wa nchi hii inayokumbwa na mashambulizi ya kundi la Kiislam la Al Shabab, baada ya mchakato wa uchaguzi uliogubikwa na tuhuma za rushwa na wizi wa kura.
Imechapishwa:
Huu ni uchaguzi ambao si kama uchaguzi unaoshuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani. Wabunge 275 na Maseneta 54 watachagua rais mpya kati ya wagombea ishirini na tatu. Uchaguzi huu si kama uchaguzi wa kawaida ambapo raia humchagua rais wao, bali raia kupitia wawakilishi wao Bungeni na katika Baraza la Seneti watamchagua rais wao mpya. Ni vigumu nchini Somalia kuandaa uchaguzi wa moja kwa moja ambapo raia humchagua rais wao. Nchi hii inatoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miongo miwili na wanajihadi wa kundi la Al Shabab wanaendelea kushambulia miji mikubwa.
Wakati huo huo milipuko imesikika katika mji Mkuu wa Somalia, Mogadishu, usiku wa kuamkia leo.
Kumekuwa na taarifa kuwa mizinga imelipuliwa karibu na uwanja wa ndege ambapo uchaguzi unatarajiwa kufanyika, huku wakazi wa eneo la Waberi iliyoko Kusini Magharibi mwa Mogadishu pia wakithibitisha kusikia milipuko hiyo.
Kufikia sasa hakuna maafa au majeruhi walioripotiwa ingawa hali ya wasiwasi imetanda katika mji wa Mogadishu.
Babarabara zote zimefungwa. Shughuli zote katika uwanja wa ndege zimesitishwa. Na hata wakazi wengine hawawezi kuvuka kutoka barabara hii hadi nyingine.
Uchaguzi huu umekuwa ukiahiarishwa mara kwa mara tangu mwezi Agosti mwaka uliopita, hasa kwa sababu za kiusalama lakini pia baada ya kucheleweshwa pia kwa uchaguzi wa wabunge.
Wagombea wengine ni pamoja na Waziri Mkuu Omar Abdirashid Sharmarke, rais wa zamani wa serikali ya mpito Sheikh Sharif Ahmed na aliyekuwa Waziri Mkuu wake Mohamed Abdullahi Farmaajo.
Wagombea wote 23 ni wanaume baada ya mgombea pekee wa kike kujiondoa mwaka uliopita.
Kila mgombea amelipa Dola za Marekani 30,000 kama ada ya kushiriki katika uchaguzi huu muhimu.
Atakayechaguliwa atakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa usalama unarejea nchini humo kutokana na tishio la Al Shabab, lakini pia kukabiliana na baa la njaa.
Suala la ufisadi pia limeendelea kuwa sugu nchini humo.