DRC-SIASA- MAZUNGUMZO

Jumuiya ya kimataifa yaelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kisiasa DRC

Tangu kusainiwa kwa mkataba wa kisiasa chini ya mwamvuli wa Braza Kuu la Maskofu wa Kanisa Katoliki nchini DR Congo (Cenco) , hakuna maendeleo thabiti juu ya utekelezaji wake.
Tangu kusainiwa kwa mkataba wa kisiasa chini ya mwamvuli wa Braza Kuu la Maskofu wa Kanisa Katoliki nchini DR Congo (Cenco) , hakuna maendeleo thabiti juu ya utekelezaji wake. Photo MONUSCO/ John Bompengo

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa “Francophonie”, zimeguswa kutokana na kuendelea kuchelewa kwa mazungumzo kuhusu utekelezaji wa makubaliano ya suluhu ya kisiasa nchini DR Congo.

Matangazo ya kibiashara

Taasisi hizo pia zimeelezea wasiwasi wao kutokana na kuendelea kusuasua kwa mazungumzo ya utekelezaji wa mkataba wenyewe, hali iliyochangiwa pakubwa pia kutokana na kifo cha aliyekuwa kinara wa upinzani Ettienne Tshisekedi ambaye alifariki majuma kadhaa yaliyopita.

Hayo yakijiri siku moja baada ya Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kudai, Serikali ya DRC haina fedha za kuandaa uchaguzi mkuu mwaka huu, waziri huyohuyo ameibuka na kudai kuwa alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari, wakati aliposema serikali haina fedha za kuandaa uchaguzi.

Waziri Pierre Kangudiya sasa anasema kuwa alichomaanisha ni kuwa, serikali haina uwezo wa kupata kiasi cha Dola Bilioni moja kwa wakati huu, na kwamba hakuwa na maana uchaguzi usifanyike nchini humo mwaka huu.

Kauli yake ya hapo jana ilizua mijadala mikali kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha wanasiasa na taasisi za kimataifa kuonesha kushangazwa na tangazo lake, ambalo walisema litadumaza juhudi ambazo zimefikiwa hadi sasa.