AFRIKA KUSINI-ZUMA-SIASA-UCHUMI

Zuma amfuta kazi Waziri wa Elimu ya Juu

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akabiliwa na kashfa za rushwa nchini mwake.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma akabiliwa na kashfa za rushwa nchini mwake. REUTERS/Mike Hutchings

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, Jumanne hii, amememfuta kazi Waziri wa Elimu ya Juu, ambaye mmoja wa wakosoaji wake wakuu, na kuonya maafisa wengine kutoka chama chake cha ANC na wale wa upinzani.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Elimu ya Juu Blade Nzimande, ambaye ni mwanachama wa chama cha SACP, mshirika wa kihistoria wa chama cha Zuma cha ANC, alionekana katika miezi ya hivi karibuni mkosoaji mkubwa wa Jacob Zuma, anayekabiliwa na kashfa za rushwa.

"Tunahisi kuwa tumesalitiwa. Chama cha ANC kinaiba mchana kweupe, " Nzimande alisema mnamo mwzi Julai.

Mbali na kufukuzwa kwa Nzimande, mabadiliko katika serikali yaliyotangazwa Jumanne hii yamewashangaza wengi kuona Waziri wa Usalama David Mahlobo kuteuliwa kwenye Wizara ya Nishati.

Chama cha SACP kilizindua maandamano ya kupinga nia ya Jacob Zuma ya kuanzisha mpango tata wa ujenzi wa vituo vya nyuklia, kwa sababu ya gharama zake.

Chama cha SACP kimelaani uamuzi wa kufukuzwa kwa Bw. Nzimande na kumshtumu rais Zuma "kuendelea vituko vyake katika utawala wa kiimla".

Katibu mkuu wa chama cha ANC Gwede Mantashe mwenyewe ameelezea masikitiko yake ya kufukuzwa kwa Nzimande.

Zuma aliwahi kufanya mabadiliko katika serikali yake manamo mwezi Machi kwa kumfuta kazi mkosoaji wake mwingine, Waziri wa Fedha Pravin Gordhan.

"Mabadiliko haya katika serikali hayana uhusiano wowote na utawala bora (...) Jacob Zuma anawafuta kazi wapinzani wake na kuwateua wafuasi wake kwa ajili ya mkutano wa chama cha ANC," amesema kiongozi wa upinzani Mmusi Maimane (Democratic Alliance).

Mnamo mwezi Desemba, chama cha ANC kitamchagua mrithi wa Zuma, ambaye atakuwa rais wa Afrika Kusini ikiwa chama hiki kitaibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2019.

Uchaguzi huu umekigawa chama cha Nelson Mandela cha ANC, madarakani tangu uchaguzi wa kwanza wa wazi nchini humo mwaka1994.

Bw Zuma anaunga mkono aliye kuwa mke wake Nkosazana-Zuma Dlami dhidi ya Makamu wa Rais, Cyril Ramaphosa, anayeungwa mkono na chama cha SACP na muungano mkuu wa vyama vya wafanyakazi nchini humo (Cosatu).