CEMAC-UHURU-UCHUMI

Jumuiya ya nchi za Afrika ya Kati yapata viongozi wapya

Daniel Ona Dondo, Mwenyekiti mpya wa tume ya Cemac. Hapa alikua bado akihudumu kama waziri mkuu katika serikali ya rais Ali Bongo Ondimba nchini Gabon, Januari 11, 2015.
Daniel Ona Dondo, Mwenyekiti mpya wa tume ya Cemac. Hapa alikua bado akihudumu kama waziri mkuu katika serikali ya rais Ali Bongo Ondimba nchini Gabon, Januari 11, 2015. AFP PHOTO / Steve Jordan

Viongozi wa Jumuiya ya nchi za Afrika ya Kati (Cemac) wametamatisha mkutano wao jijini Njamena nchini Tchad, mkutano ambao ulitumiwa zaidi kuhusu maswala ya uhuru wa usafiri kwa wananchi wa mataifa hayo, lakini pia uteuzi wa mwenyekiti wa Cemac.

Matangazo ya kibiashara

Profesa Daniel Ona Ondo waziri mkuu wa zamani katika serikali ya rais Ali Bongo Ondimba nchini Gabon, ndie ambae amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa tume ya Cemac huku Fatima Haram Acyl wa Tchad ndie ameteuliwa kuwa naibu wake.

Mbali na hao viongozi wa Jumuiya hiyo wamewateuwa pia wakuu wa taasisi mbalimbali za Cemac, hivyo waziri mkuu wa zamani nchini Tchad Nagoum Yamassoum anakuwa rais wa Cosumaf, taasisi inayohusika na ufuatiliaji wa masoko katika Jumuiya hiyo.

Ili kuharakisha hatuwa zilizochukuliwa katika mkutano huo wa Ndjamena, wakuu wa nchi waliamua kutoa faranga za CEFA bilioni moja zitazosaidia kuwezesha kuanzishwa kwa vifaa vya kiufundi kwa harakati usafiri huru katika nchi wanachama.

Hata hivyo ili kuendeleza Jumuiya hiyo, inahitajika pesa, viongozi hao wameafikiana kuhusu malimbikizo ya michango ya nchi sita wananchama ambayo yanakadiriwa kufikia asilimia 90 kuyalipa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa 2017

Majadiliano yanaendelea baina ya Cemac na Umoja wa Ulaya ambae ndie mfadhili mkuu ambae amekuwa akituhumu Jumuiya hiyo kutokuwa mfano mzuri katika swala la uhuru wa watu kutembea na mali zao katika nchi za jumuiya hiyo. Baada ya Tchad na jamuhuri ya Afrika ya kati, Gabon na Equatorial Guinea zimetangaza kuondowa visa kwa wananchi wa mataifa wanachama.